Saturday, December 2, 2017

HALMASHAURI WILAYA YA MBINGA KUONGEZA VITUO VYA KUTOLEA HUDUMA ZA AFYA KARIBU NA WANANCHI

Mbunge wa jimbo la Mbinga vijijini, Martin Msuha akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kipololo wilayani Mbinga siku ya maadhimisho ya Ukimwi duniani ambapo alisisitiza kwa kuwataka wananchi hao wajitokeze kwa wingi kupima afya zao ili waweze kujitambua kama wameambukizwa au la. 

Ngoma mbalimbali za asili ikiwemo mganda wananchi walijitokeza kwa wingi kucheza ngoma hizo na kuhamasisha wenzao kupima afya zao.

Afisa maendeleo ya jamii, Davina Maketa akitoa elimu namna ya kujikinga na maambukizi mapya ya Virusi vya ukimwi, kwa wananchi wa kata ya Kipololo ambao walijitokeza siku ya maadhimisho ya ukimwi duniani ambayo yalifanyika katika kata hiyo.
Na Kassian Nyandindi,     
Mbinga.

IMEELEZWA kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, imejiwekea mikakati ya kuendelea kuongeza vituo vya huduma za afya karibu na wananchi ikiwemo kuhimiza kila kijiji, kuwa na mpango mkakati wa kuwasaidia watu wake walioathirika na ugonjwa wa ukimwi.

Aidha mkakati mwingine walionao, kulinda haki za watu wanaoishi na Virusi Vya Ukimwi (VVU) na kifua kikuu pamoja na kupunguza vitendo vya unyanyapaa ambavyo vimekuwa vikijitokeza katika jamii dhidi ya watu walioathirika na ugonjwa huo.

Hayo yalisemwa jana na Henry Digongwa ambaye ni Mratibu wa ukimwi wilayani hapa, katika maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani wakati alipokuwa akisoma taarifa ya utekelezaji na mikakati iliyojiwekea halmashauri hiyo katika kupambana na ugonjwa huo.


Maadhimisho hayo katika halmashauri ya wilaya ya Mbinga yalifanyika katika kijiji cha kipololo kata ya Kipololo ambapo ni jukumu la jamii kuhakikisha kwamba inaepukana na maambukizi mapya ya virusi hivyo.

Digonjwa alifafanua kuwa wananchi wanapaswa pia kuendelea kupambana na janga hilo kwani idara ya maendeleo ya jamii wilayani humo, itahakikisha inaendelea kutoa elimu ya kinga na maambukizi ya virusi vya ugonjwa huo kwa wananchi wote ambao hawajitokezi kupima afya zao ili waweze kujitambua na wabaki salama.

Alisema kuwa katika hilo watahimiza pia upimaji wa VVU kwa hiari, kutoa ushauri nasaha na kuelimisha jamii waweze kuondokana na vitendo vya unyanyapaa dhidi ya watu waliothirika na virusi vya ukimwi.

Kadhalika katika wilaya ya Mbinga kwa mwaka 2016 watu wapatao 61,394 walijitokeza kupima afya zao kwa hiari wakiwemo wanaume 29,218 na wanawake 32,176 ambapo kati yao waliokutwa na maambukizi walikuwa 1,393 wakiwemo wanaume 585 na wanawake 808.

Aliongeza kuwa maambukizi hayo ni sawa na asilimia 2.6 hivyo jamii inatakiwa kuchukua tahadhari ya kujikinga na maambukizi mapya.

Kwa upande wake mgeni rasmi wa maadhimisho hayo, Martin Msuha ambaye ni Mbunge wa jimbo la Mbinga vijijini aliwataka wananchi waachane na vitendo vya ngono zembe, huku akiwataka wanaume kujitokeza kwa wingi kufanya tohara ili kuweza kuzuia maambukizi hayo.

Pia Msuha alisisitiza kwamba kwa wale ambao wataonekana kuwa na maambukizi wazingatie tiba huku akieleza kuwa changamoto tuliyonayo katika jamii hivi sasa, kumekuwa na baadhi ya watu kutozingatia taratibu za umezaji wa dawa za kufubaza virusi vya ukimwi hivyo kusababisha virusi hivyo kuwa sugu.

Hata hivyo alibainisha kuwa Serikali itaendelea kuzuia maambukizi ya mama kwenda kwa mtoto na kufanya juhudi ya kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu katika kupima afya zao ili waweze kujitambua kama wameathirika au la.

No comments: