Na Muhidin Amri,
Tunduru.
MGANGA Mkuu wa wilaya ya Tunduru
mkoani Ruvuma, Dokta Wendy Robert amesema kuwa idara ya afya katika wilaya hiyo
itaanza kupima afya za wananchi wanaotoa huduma ya kuuza chakula katika maeneo
mbalimbali wilayani humo.
Akizungumza juzi na baadhi ya watoa
huduma alisema kuwa lengo la mpango huo ni kuhakikisha kuwa kila mtoa
huduma anakuwa na afya njema, ili kuepusha uwezekano wa kuambukiza wateja wao
hasa pale wanapowahudumia ili kupata watu wenye afya njema watakaoweza kushiriki
moja kwa moja katika kazi za maendeleo.
Aidha alisema kuwa zoezi hilo
litafanyika kwa wilaya yote ya Tunduru katika migahawa, hoteli na maeneo
mengine kwani wapo baadhi ya watoa huduma kama vile kwenye migahawa bado
hawajapimwa afya zao jambo linaloweza kuhatarisaha maisha ya watu wengine.
“Unapokuwa na matatizo ya kiafya kama
vile TB na magonjwa mengine ni rahisi kuambukiza watu wengine kwa njia ya hewa,
kwa hiyo tunataka kuhakikisha kwamba watoa huduma wote wa chakula wanakuwa na
afya njema”, alisema Dokta Robert.
Katika utekelezaji wa mpango huo, alisema
timu ya wataalamu wa afya itatembelea katika kila kata ili kuweza kuleta
ufanisi wakati wa utekelezaji wa zoezi hilo na kwamba wamiliki wa migahawa na
hoteli wametakiwa pia kuwafanyia uchunguzi wa afya wafanyakazi wao mara kwa
mara.
No comments:
Post a Comment