Friday, December 8, 2017

SERIKALI IPO KATIKA MCHAKATO WA KUMTAFUTA MKANDARASI UJENZI BARABARA KIWANGO CHA LAMI MBINGA KWENDA NYASA

Na Mwandishi wetu,    
Songea.

IMEELEZWA kuwa taratibu za ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kutoka Mbinga mjini kuelekea wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, zinaendelea ambapo hivi sasa Serikali inafanya kazi ya kumtafuta Mkandarasi ambaye atafanya kazi hiyo.

Mkuu wa Mkoa huo, Christine Mndeme alisema hayo juzi wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa.

“Serikali inaendelea kulifanyia kazi jambo hili, taratibu za kumpata mkandarasi zinaendelea ujenzi utafanyika wananchi wasiwe na wasiwasi”, alisema Mndeme.

Aliongeza kuwa malengo ya Serikali katika kutekeleza kazi hiyo ya ujenzi wa barabara ya kutoka Mbinga mjini kwenda Nyasa yapo na sio vinginevyo.

Pamoja na mambo mengine, wananchi wamekuwa wakilalamikia na kuhoji juu ya ujenzi wa barabara hiyo kwamba imekaa kwa muda mrefu hakuna utekelezaji unaofanyika, tofauti na maelezo ya Serikali waliyoelezwa hapo awali kwamba kiangazi cha mwaka huu 2017 kabla ya mvua za masika kuanza kunyesha ujenzi huo ungeanza kufanyika.

Wananchi hao walidai kuwa viongozi wa Serikali walipokuwa wakiwatembelea na kufanya ziara zao za kikazi, walikuwa wakisisitiza kwa kuwaeleza kuwa barabara hiyo itajengwa lakini wanashangaa kuona ni muda mrefu unapita barabara hiyo haijengwi.

Pia walieleza kuwa wanaiomba Serikali ichukue hatua ya kuijenga haraka kwa kiwango hicho ili waweze kuondokana na kero wanayoipata sasa ya kusafirisha bidhaa zao hasa katika kipindi cha masika.

No comments: