Monday, December 4, 2017

TUNDURU WATAKIWA KUZINGATIA KANUNI BORA ZA KILIMO CHA KOROSHO

Zao la Korosho.
Na Dustan Ndunguru,     
Tunduru.

MKUU wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, Juma Homera amewataka wakulima wa korosho wilayani humo kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa kilimo kuhusiana na njia sahihi za utunzaji wa zao hilo, ili hatimaye waweze kuzalisha mazao yenye ubora kwa wingi yenye bei nzuri sokoni.

Homera alisema kuwa katika kipindi cha msimu wa mavuno mwaka huu wakulima wameweza kupata bei nzuri hivyo wanapaswa kuhakikisha kwamba wanaendelea kuboresha njia za uzalishaji ili bei izidi kuongezeka na kuwafanya waweze kujikwamua kiuchumi.

Alisema hayo alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hizi ambapo aliongeza kuwa wakulima msimu huu wamefanikiwa kuuza Korosho zao kwa bei ya shilingi 4,010 ikiwa ni mwaka wa pili mfululizo ambapo wamekuwa wakiuza kupitia mfumo wa stakabadhi ya mazao ghalani ambao una manufaa makubwa kwa wakulima.

Vilevile aliipongeza kampuni ya Sunshine Tanzania Limited na Export Trading Tanzania Limited kwa kuibuka vinara wa kununua korosho za wakulima hao kwa bei ya juu, kati ya makampuni 11 yanayonunua wilayani humo.

Naye Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Tunduru, Chiza Malando alisema kuwa wakulima wanatarajia kuvuna zaidi ya tani 20,000 katika msimu wa mwaka 2017/2018 na kwamba anayo imani kuwa korosho zote zitauzwa kupitia mfumo huo wenye manufaa makubwa kwa wakulima.

Malando alitumia nafasi hiyo kuyahimiza pia makampuni yaliyonunua Korosho hizo kuwalipa haraka wakulima hao ili waanze kuyaona manufaa ya kazi waliyofanya.

Nao wakulima wa kutoka katika Kijiji cha Amani kilichopo kata ya Mtina, tarafa ya Lukumbule, Halifa Lilombea, Mussa Athumani na Zainabu Baisi Yasini kutoka kijiji cha Mchoteka kwa nyakati tofauti waliipongeza Serikali kwa kubuni mfumo huo wa stakabadhi ya mazao ghalani kutokana na kuwapatia bei nzuri ambayo hawajawahi kuipata tangu waanze kulima na kuuza korosho.

Walisema ingawa awali mfumo huo ulionekana kuwa na mapungufu madogo madogo na kuwafanya wakulima kuukataa lakini kuanzia sasa hakuna mkulima atakayeweza kupinga, kutokana na Serikali kuufanyia marekebisho na kwamba hakuna mtu anayeweza kujitokeza na kuwaibia wakulima kama ilivyokuwa hapo awali.

Mwenyekiti Chama kikuu cha ushirika wakulima wa korosho wilayani Tunduru (TAMCU) Hashim Mbarabara, aliwaasa wakulima wa zao hilo kutumia vizuri fedha watakazozipata ikiwemo kupeleka watoto wao shule, kujenga nyumba bora za kisasa na kununua pembejeo ambazo zitawasaidia kuhudumia mashamba yao katika msimu ujao.

No comments: