Na Muhidin Amri,
Madaba.
UJENZI wa mabweni ya kulala Wanafunzi
katika shule ya Sekondari Mahanje, Halmashauri ya Wilaya ya Madaba Mkoani
Ruvuma utasaidia kwa kiasi kikubwa kumaliza kero ya watoto wanaosoma katika
shule hiyo kutembea umbali mrefu wa kilometa 12 kutoka majumbani kwao hadi
shuleni.
Hivi sasa ujenzi huo ambao unaendelea
kufanyika ni wa mabweni mawili makubwa yanajengwa ambayo kila moja litakuwa na
uwezo wa kulaza watoto 80.
Shule hiyo ambayo ni ya wasichana na
wavulana, yanajengwa majengo hayo kwa ajili ya kulaza watoto hao ambayo sasa
yamefikia hatua ya mwisho kukamilika kwake na kwamba, yataweza pia kusaidia
hata wanafunzi hao wasiweze kupoteza muda wao wa kuhudhuria ipasavyo vipindi
vya masomo darasani.
Mbali na kumaliza kero hiyo mabweni hayo
yatasaidia kuongeza ukuaji wa taaluma kutokana na watoto wengi wataishi katika
mazingira ya shule na kupata muda mwingi wa kujisomea tofauti na ilivyokuwa
sasa.
Mkuu wa shule hiyo, Marcelino Kilewa
alisema Serikali imetoa jumla ya shilingi milioni 196.8 kwa ajili ya ujenzi wa
mabweni hayo, vyumba viwili vya madarasa na matundu ya choo katika shule hiyo.
Alisema kuwa katika mwaka wa masomo
2018, shule hiyo inatarajia kupokea wanafunzi waliochaguliwa kuingia kidato cha
kwanza 135 na tayari kuna wanafunzi 247 ambao wanasoma wakitokea majumbani
kwao.
Kwa upande wake Afisa elimu Sekondari
wa halmashauri ya wilaya ya Madaba, Davis Mwasi aliongeza kuwa mradi huu wa ujenzi
wa mabweni mawili, madarasa na matundu ya vyoo unalenga zaidi kuinua maendeleo
ya elimu kwa watoto hao.
Alisema kuwa Serikali imetoa fedha
hizo ambapo miundombinu hiyo ujenzi wake umefikia hatua nzuri na halmashauri hiyo
tayari imejipanga kwa kila shule ya Sekondari wilayani humo kunakuwa na mabweni
ya kutosha kwa ajili ya kulala wanafunzi.
Hata hivyo Afisa elimu huyo
amempongeza Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Madaba, Shafi Mpenda kwa
juhudi zake anazozifanya za ufuatiliaji na usimamizi mzuri wa miradi ya
maendeleo ya wananchi ambayo inatekelezwa katika maeneo mbalimbali wilayani hapa.
No comments:
Post a Comment