Na Dustan Ndunguru,
Songea.
MKUU wa mkoa wa Ruvuma Christine Mndeme
amewataka maofisa ugani na wataalam wa masuala ya kilimo mkoani humo, kuhakikisha
kwamba wanasimamia kwa ukaribu maandalizi ya uzalishaji mazao mbalimbali,
katika msimu wa kilimo mwaka 2017/2018 ili wakulima waweze kuzalisha mazao
mengi na yenye ubora ambao utawafanya wapate bei nzuri sokoni.
Mndeme alitoa agizo hilo juzi alipokuwa
akifungua kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa, kilichofanyika kwenye ukumbi wa Manispaa ya Songea mjini hapa.
Alisema kuwa msimu wa mvua kwa mwaka
2017/18 umeanza ambapo wakulima wanapaswa kwenda mashambani ili waweze kupata
mafanikio katika kazi wanayofanya ya uzalishaji wa mazao mbalimbali.
Alisisitiza kuwa ni muhimu kwa
wataalamu wa kilimo kuwatembelea mara kwa mara wakulima hao na kuwapa maelekezo
ya kitaalamu namna ya kuzingatia kanuni bora za kilimo.
“Mvua hivi sasa zimeanza kunyesha,
kuashiria kazi ya kilimo kuanza hivyo jukumu la maofisa ugani ni kihakikisha
wanawafuata wakulima vijijini na kuwapa elimu ya namna bora ya uzalishaji wa
mazao yao ili waweze kuzalisha kwa tija”, alisema.
Mkuu huyo wa mkoa alifafanua kuwa
kuanzia msimu huu wa kilimo Serikali haitatumia mfumo wa pembejeo za ruzuku
kama ilivyozoeleka katika kipindi cha miaka ya nyuma badala yake wakulima
watanunua mbolea kwa bei elekezi itakayotolewa na Wizara ya kilimo.
Alibainisha kuwa lengo la utaratibu
huo wa kutumia bei elekezi itakayotolewa ni kuweza kuwafanya wakulima waweze
kupata mbolea za kupandia na kukuzia mazao yao shambani.
Vilevile aliongeza kuwa mfumo huo utawezesha
wakulima wengi mkoani Ruvuma kuzalisha mazao mengi kama vile mahindi na kwamba aliwaagiza
Wakuu wa wilaya na Wakurugenzi wa mamlaka za Serikali ya mitaa katika mkoa huo,
kusimamia kikamilifu zoezi hilo mara Serikali itakapotoa maelekezo husika.
Mkoa huo ni moja kati ya mikoa
inayozalisha mazao mengi ya chakula na biashara hapa nchini ikiwemo mahindi
ambapo katika msimu wa 2016/2017 ulivuna jumla ya tani milioni
1,232,776 za mazao ya chakula aina ya wanga ambapo mahitaji halisi ya
chakula ni tani 338,889 na kuufanya mkoa kuwa na ziada ya chakula tani
893,887.
Aliwataka wakulima kuzitumia vizuri
mvua zinazoendelea kunyesha kwa kuzalisha mazao kwa wingi na kwamba wahakikisha
wanazingatia maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa kilimo kwenye maeneo yao
badala ya kulima bila kuzingatia utaalamu hali ambayo husababisha wavune mazao
kidogo yasiyo na ubora unaotakiwa kwenye masoko.
No comments:
Post a Comment