Na Kassian Nyandindi,
Songea.
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewatoa
hofu wakazi 1,000 wa Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma ambao wanadai fidia ya shilingi
bilioni 3.8 ya eneo lao ambalo limechukuliwa na kuwa eneo la kiuchumi mkoani humo
(Ruvuma SEZ) kwa ajili ya ujenzi wa viwanda.
Amewatoa hofu jana wakati
alipokuwa akizungumza na wakazi wa kata ya Mwengemshindo katika mkutano wa
hadhara uliofanyika kwenye Manispaa hiyo.
Majaliwa alisema kuwa Serikali ya
awamu ya tano inatambua kilio chao ambacho alisema ni cha muda mrefu na kwamba alishawahi
kupata ombi maalum kutoka kwa Mbunge wao wa zamani, Leonidas Gama ambaye sasa
ni marehemu ili kuweza kumaliza jambo hilo.
“Alipotoka kutibiwa India alikuja Ofisini
kwangu na kunieleza kwamba ana mambo mawili ambayo nikifanya ziara mkoani
Ruvuma anaomba niyatafutie ufumbuzi, la kwanza lililkuwa ni hili la fidia kwa
wakazi wa Mwengemshindo na la pili lilikuwa ni la ujenzi wa kituo cha mabasi
cha mjini Songea,
“Leo nimefanya ziara maalum kwa ajili
yenu kwa sababu Serikali ya awamu ya tano ipo kwa ajili yenu na hasa wananchi
wanyonge na tatizo hili inalijua kabla sijafika hapa, nilipita kwenye eneo
husika na afisa mipango miji akanionyesha ramani ya eneo lenu hili”, alisema Majaliwa.
Waziri Mkuu huyo aliwaeleza pia wakazi hao
kwamba eneo hilo limetengwa na Manispaa kwa ajili ya ujenzi wa viwanda ambapo
wawekezaji watatu tayari wamekwishajitokeza na wanataka kujenga viwanda
vitatu.
Alieleza kuwa kutakuwa na kiwanda cha
kusindika mahindi, kutengeneza pumba za kuku na ng’ombe na mbolea na kwamba kiwanda
cha pili kitakuwa ni cha kusindika kahawa na cha tatu kitakuwa ni cha kukamua
mafuta ya mbegumbegu huku akiongeza kuwa hata ujenzi wa reli ya kutoka Mtwara kwenda
Mbamba bay wilayani Nyasa mkoani hapa inatarajiwa kupita kwenye eneo hilo.
Vilevile akitoa ufafanuzi juu ya kuchelewa
kwa malipo yao, Waziri Mkuu Majaliwa alisema kwamba kati ya wawekezaji hao
watatu aliyekwishalipa fidia ni mmoja tu na kwamba kwa mujibu wa sheria ya
uwekezaji, fidia inapaswa kulipwa na mnunuzi wa eneo husika.
Kadhalika alikiri kuwepo kwa
mapungufu wakati wa ulipaji huo kwa sababu walifuata orodha ya majina (Kialfabeti)
badala ya kutoa malipo kwa wakazi wa eneo husika.
“Sasa hivi mwekezaji anataka kuanza
ujenzi, lakini ndani ya eneo lake kuna watu ambao bado hawajalipwa, kwa hiyo
hawawezi kutoka hadi wale waliobakia nao walipwe, Serikali itawafuatilia hawa
wawekezaji wengine ili nao walipe fedha zao haraka ili waliobakia waweze
kulipwa”, alisema.
Jumla ya watu 2,179 walifanyiwa
uthamini mwaka 2008 na gharama yao kubainika kuwa ni shilingi 3,254,737,622
ambapo kuanzia Juni 8-19, 2015, Serikali iliwalipa wakazi 1,179 shilingi 1,920,242,121
ambapo kati ya hizo, shilingi 1,210,078,261 zilikuwa ni malipo ya thamani ya
mali za wananchi na shilingi 710,163,860 zilikuwa ni riba kutokana na malipo
hayo kuchelewa kufanyika.
Eneo hilo lenye ukubwa wa hekta 2,033
(Sawa na ekari 5,000) lilitwaliwa na Mamlaka ya Ukanda Maalum wa Uwekezaji
(EPZA) kwa kushirikiana na uongozi wa mkoa wa Ruvuma na Manispaa ya Songea
tangu mwaka 2007 na kwamba eneo hilo linajumuisha mitaa ya Luwawasi (Mkuzo),
Mwengemshindo na Luhira.
No comments:
Post a Comment