Na Muhidin Amri,
Tunduru.
DEREVA anayejulikana kwa jina la Dastan
Mpepo aliyekuwa akiendesha gari aina ya Nissan Forward lenye namba za usajili T
779 ASC anatafutwa na Jeshi la Polisi mkoani Ruvuma kwa tuhuma ya kusababisha
mauaji Wilayani Tunduru mkoani humo.
Akizungumza na waandishi wa habari
Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Gemini Mushi alisema kuwa tukio hilo lilitokea
Desemba 9 mwaka huu majira ya saa 3:30 usiku baada ya dereva huyo kugongana uso
kwa uso na mwendesha Pikipiki aliyetambuliwa kwa jina la Yusto Seleman Mtega
(43) ambaye ni Meneja wa Kampuni ya ulinzi Komesha Security iliyopo Tunduru
mjini.
Kamanda Mushi alifafanua kuwa baada
ya Meneja huyo kugongwa na gari hilo katika eneo la Kona ya mbwa iliyopo mjini
hapa dereva alitekeleza gari lake na kutokomea kusikojulikana.
Alisema kuwa Mtega kabla ya kukutwa
na umauti alikuwa akiendesha Pikipiki hiyo aina ya Sunlg akielekea nyumbani
kwake ambako anaishi katika mtaa wa Biasi.
Kamanda Mushi amewataka wanachi ambao
watapata taarifa ni wapi dereva Mpepo amekimbilia watoe taarifa kwa Jeshi la
Polisi ili waweze kumpata mtuhumiwa huyo na sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Kwa upande wake akizungumzia taarifa
za tukio hilo Meneja msaidizi wa kampuni hiyo, Said Kaondo Issa alisema kuwa
marehemu aligongwa katika barabara ya Tunduru-Namtumbo katika eneo la mtaa wa
Kona ya mbwa wakati anaelekea nyumbani kwake muda mfupi baada ya kukamilisha
majukumu yake ya kazi ya kuwasambaza askari wa kampuni hiyo kwenda katika maeneo
ya malindo ambako wanafanya kazi.
Alisema kufuatia hali hiyo tayari
amekwisha wasiliana na Mkurugenzi wa kampuni kwa ajili ya kuangalia uwezekano
wa kusafirisha mwili wa marehemu kuelekea katika kijiji cha Lupanga kilichopo Wilaya
ya Ludewa kwa ajili ya taratibu za mazishi.
Dokta Titus Tumbu ambaye ni Mganga
aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu huyo, alisema kuwa chanzo cha kifo
hicho kilitokana na ubongo wake kupata mkandamizo na kupasuka kwa fuvu la
kichwa baada ya kugongwa na gari hilo.
Pia Dokta Tumbu aliongeza kuwa katika
tukio hilo marehemu aliumia vibaya kwa kuvunjika miguu yote miwili pamoja na
mkono wa kushoto.
No comments:
Post a Comment