Na Muhidin Amri,
Tunduru.
SERIKALI imeyataka mabenki yanayotoa
huduma Wilayani Tunduru mkoani hapa, kuandaa utaratibu wa kupeleka huduma hizo
vijijini ikiwa ni juhudi ya kusogeza huduma hizo karibu na wananchi.
Agizo hilo lilitolewa na Mkuu wa wilaya
hiyo, Juma Homera wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mchoteka wilayani
humo waliojitokeza katika shughuli ya Mnada wa sita wa kuuza zao la korosho
uliofanyika katika Chama cha ushirika cha wakulima Litunguru Amcos.
Homera alilazimika kutoa ushauri huo,
baada ya kubaini uwepo wa uhitaji wa huduma hiyo kwa wananchi hasa wakati huu
wa mauzo ya zao hilo.
Alisema endapo mabenki hayo
yatashindwa kutekeleza agizo hilo kwa wakati watafute mawakala watakao weza kuwakilisha
utendaji kazi wa benki hizo katika maeneo hayo ili kuwaondolea adha wakulima wa
korosho ambao hivi sasa wamekuwa wakisafiri umbali mrefu kufuata huduma hiyo
Tunduru mjini.
Awali akitoa maelekezo ya mnada huo Kaimu
Meneja wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) tawi la Tunduru, Jafari Matata alisema
minada hiyo hufanyika baada ya chama kikuu cha ushirika wilayani Tunduru
(TAMCU) kusambaza vijarida vinavyoonesha ubora na idadi ya kiasi cha kilo za
korosho zitakazouzwa katika mnada husika kwa wanunuzi wote.
Matata alieleza kuwa baada ya
kukamilika kwa taratibu hizo za kisheria wanunuzi huandika barua za kuomba
kununua Korosho hizo wakiwa wameainisha bei na kiasi wanachokihitaji, ambapo
wakati wa mnada husika barua hizo husomwa mbele ya wakulima na kutoa nafasi
kwao kuchagua bei iliyowaridhisha na kuridhia kuuza korosho zao.
Baada ya kutolewa kwa maelekezo hayo
wakulima hao huridhia kuuza korosho zao kwa bei ya wastani wa shilingi 3,771.49
kwa kila kilo moja ya korosho ambayo ilikuwa imeingizwa katika maghala ya
kuuzia.
Akitoa taarifa za mauzo ya mnada huo
naye Meneja wa chama kikuu cha ushirika wilayani Tunduru (TAMCU) Imani Kalembo
alisema kuwa katika mnada huo jumla ja tani 2,538 zilipangwa kuuzwa katika
mnada huo.
Hata hivyo baada ya wakulima kuridhia
kuuza kiasi hicho cha tani 2,538 chama hicho kimefikisha jumla ya mauzo ya tani
16,281.683 za korosho zilizokusanywa kutoka kwa wakulima wilayani humo katika
msimu huu wa mwaka 2017/2018.
No comments:
Post a Comment