Na Muhidin Amri,
Mbinga.
JUMLA ya Wakazi 100 wa kijiji cha Kigonsera kata ya Kigonsera
Halmashauri ya wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wamefikishwa Mahakamani kwa kosa
la kukataa kushiriki katika shughuli za maendeleo ikiwemo ujenzi wa mabweni ya
wanafunzi.
Hayo yalisemwa juzi na Mtendaji wa kata ya Kigonsera, Raphael
Kalembo wakati alipokuwa akizungumzia ujenzi wa nyumba moja ya walimu katika
shule ya Sekondari ya Kigonsera ambayo ujenzi wake ukikamilika, itakuwa na
uwezo wa kuishi walimu watakaoweza kufanya kazi ya kufundisha katika shule
hiyo.
Ujenzi wa nyumba hiyo ni mkakati wa uongozi wa shule kwa
kushirikiana na halmashauri hiyo kutatua kero ya nyumba za kuishi walimu hao katika
halmashauri ya wilaya ya Mbinga.
Kalembo alisema kuwa kati ya hao tayari wengine wamekwisha
hukumiwa vifungo na baadhi wamelipa faini kama hatua ya kuwataka kutambua
majukumu na umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika kazi za ujenzi wa taifa.
Alisema kuwa kazi ya ujenzi wa Taifa ni jukumu la kila mmoja
katika jamii lakini moja kati ya changamoto zinazoikabili kata hiyo ni baadhi
ya wananchi kukataa kushiriki shughuli za maendeleo, hivyo kusababisha kata
hiyo kuwa na miradi mingi viporo ikilinganishwa na kata nyingine.
Tatizo la upungufu wa nyumba za kuishi walimu katika shule
hiyo na shule nyingine zilizopo kwenye kata hiyo limekuwa kubwa hivyo
zinahitajika juhudi kubwa kuhakikisha kwamba wanajenga haraka nyumba za kutosha
ili kuweza kuwaondolea kero ya walimu kupanga uraiani.
Alifafanua kuwa mbali na ujenzi wa nyumba hizo halmashauri hiyo
ya wilaya inaendelea na ujenzi wa mabweni mawili ya wanafunzi katika shule ya Sekondari
Kiamili iliyopo katika kata hiyo, ambayo kila moja litakuwa na uwezo wa
kuchukua wanafunzi 48 ili kuwasaidia wasiweze kuishi mbali na mazingira ya
shule.
Kwa upande wake Kaimu Afisa mipango wa halmashauri ya wilaya
ya Mbinga, Zainabu Mfinanga alitolea ufafanuzi kuwa kazi ya ujenzi wa mabweni
hayo unaenda sambamba na ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa baadhi ya shule na
nyumba hizo za walimu katika maeneo mbalimbali wilayani humo.
No comments:
Post a Comment