Na Mwandishi wetu,
Mbinga.
WANANCHI wa wilaya ya Mbinga mkoani
Ruvuma wamesisitizwa kuzingatia kula mlo kamili ili kuweza kwenda sambamba na
mambo mbalimbali ikiwemo kuwa na afya bora kwa faida ya maendeleo ya kizazi cha
sasa na kijacho.
Vilevile imesisitizwa kuwa ulaji wa
lishe bora unapaswa uendane na mchanganyiko wa vyakula ambavyo vina wanga,
protini, mboga mboga, matunda na sukari.
Janeth Bandari ambaye ni Afisa lishe
wa Halmashauri ya wilaya hiyo alisema hayo jana wakati alipokuwa akizungumza na
wananchi wa kata ya Kipololo katika maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani.
“Tujitahidi kula mlo kamili kwa
sababu mlo bora unajenga mwili na kumfanya mtu akue vizuri kimwili hata
kiakili, binadamu unatakiwa upate lishe bora tokea pale unapozaliwa”, alisema.
Alifafanua kuwa binadamu akizingatia
hilo anaweza kumjenga mtoto wake akue vizuri tokea anapokuwa tumboni mwa mama
yake kabla ya kuzaliwa.
Pia alieleza kuwa wataalamu wa
masuala ya afya wamekuwa mara kwa mara wakisisitiza hilo ili kuifanya jamii
iendane na ulaji mzuri wa vyakula ambao unajenga mwili na kuweza kuepukana na
magonjwa mbalimbali.
Pamoja na mambo mengine kwa nyakati
tofauti wananchi wa kata ya Kipololo waliunga mkono na kueleza kuwa
watazingatia hilo, kwani wao wamekuwa wakizalisha vyakula vingi vya aina
tofauti ambavyo vinafaa kwa matumizi ya binadamu katika kuujenga mwili.
No comments:
Post a Comment