Na Kassian Nyandindi,
Songea.
MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Christine
Mndeme ametoa wito kwa wazazi na wananchi wa mkoa huo kupuuza habari
zinazosambaa katika mitandao ya kijamii, kwamba amekataza watu wazima mkoani
humo marufuku kuitana baby jambo ambalo sio la kweli.
Aidha alifafanua kuwa kauli hiyo
inamlenga mwanafunzi wa kike ili aweze kufikia ndoto yake ya kumaliza masomo
anapokuwa shuleni, ambapo anapaswa kuvaa magauni manne na asikubali kuitwa baby
au mrembo na wavulana ambao huwahadaa kwa lengo la kufanya nao mapenzi na hatimaye kukatisha masomo yake.
Hayo yalisemwa juzi na Mkuu huyo wa
Mkoa wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Ikulu ndogo mjini
Songea.
Alisema kuwa kauli hiyo inamaana
kwamba, gauni la kwanza linamtaka mtoto wa kike shuleni avae sare zake za
shule, gauni la pili avae joho la mahafali, la tatu avae gauni la harusi na la
nne ndipo avae gauni la pale anapokuwa na ujauzito.
Mndeme alieleza kuwa mwanafunzi huyo anapovaa
gauni la kwanza maana yake anapaswa kuzingatia masomo yake mwanzo hadi mwisho
kwa kuhakikisha hawezi kuingia katika vishawishi vya kupata mimba ambavyo
vinakatisha ndoto yake ya kuendelea na masomo.
Vilevile kwa gauni la pili alieleza
kuwa hapo mtoto wa kike anakuwa tayari amepevuka na kuweza kuvaa gauni la tatu
ambalo ni la harusi baada ya kupa mume.
“Kauli mbiu hii nimekuwa nikiitumia
mara kwa mara na imekuwa ikinisaidia katika kupambana na mimba za utotoni hasa
kwa watoto waliokuwa shule na nina uhakika kwa mkoa huu wa Ruvuma itanisaidia sana
hivyo wanafunzi wa kike wasikubali kushawishiwa na wavulana kwa kuitwa baby na
hatimaye kukatisha masomo yao”, alisema Mndeme.
Aliongeza kuwa amesikitishwa na
baadhi ya watu ambao wamekuwa wakitafsiri kauli hiyo tofauti na alivyosema na
kuongeza kuwa malengo yake makuu ni kupambana na mimba za utotoni hasa kwa
watoto wa kike ambao wapo shuleni.
“Kitendo cha wanafunzi wa kike kuitwa
baby kikiachwa bila kukemewa miongoni mwa jamii kinaleta athari mbaya katika
makuzi ya mtoto wa kike na maendeleo yake kielimu anapokuwa shuleni, wanaume
wenye nia mbaya wamekuwa wakiwahadaa watoto hawa eti anampenda huku akimuita
baby na baada ya huingia katika vishawishi na kumsababishia ujauzito na ndiyo inakuwa
mwisho wa ndoto ya mtoto kufikia malengo yake kielimu”, alisema.
Alibainisha kuwa wakati mwingine vitendo
hivyo husababisha watoto hao kupata maambukizi ya Virusi vya ugonjwa wa ukimwi
na kusababisha vifo kwa sababu ya kuzaa katika umri mdogo.
Alisisitiza kuwa Serikali ya awamu ya
tano itaendelea kupambana na watu wenye nia mbaya wanaoshawishi watoto hao
katika umri wa kwenda shule kukatisha masomo yao baada ya kupata ujauzito.
Pamoja na mambo mengine, Novemba 8
mwaka huu Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Mndeme alitoa kauli hiyo ya kuitaka jamii
iache kuwaita watoto wa kike baby wakati alipokuwa hivi karibuni katika ziara
yake ya kikazi wilayani Namtumbo mkoani humo.
No comments:
Post a Comment