Baadhi ya Wananchi wa wilaya ya Nyasa wakiwa pembezoni mwa ziwa Nyasa. |
Songea.
TIMU ya Wataalamu wa Wizara ya afya
maendeleo ya jamii, jinsia wazee na watoto imebaini kuwa mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu
ambao umetokea katika wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma, umesababishwa na wakazi
wanaoishi katika baadhi ya maeneo ya wilaya hiyo kutozingatia kikamilifu kanuni
bora za usafi katika mazingira yao wanayoishi.
Kufuatia hali hiyo, vifo vya watu nane
vilijitokeza kutokana na ugonjwa huo kati ya wagonjwa 185 waliojitokeza
kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Liuli, Kituo cha afya Lundo, Chiulu na
Mbamba bay.
Akizungumza na waandishi wa habari
mjini hapa Mganga Mkuu wa hospitali ya mkoa huo, Dokta Gosbert Mutahyabarwa
alisema kuwa upembuzi yakinifu uliofanywa na wataalamu hao umebaini kuwa kati
ya sampuli 15 zilizochukuliwa katika maeneo ambayo ugonjwa huo umetokea,
sampuli 13 zilikuwa na vimelea vya Kipindupindu.
Dokta Mutahyabarwa alifafanua kuwa
kata ambazo zilikuwa zimeathiriwa na ugonjwa huo ni Mtipwili, Chimate na
Lipingo wilayani humo.
Alieleza kuwa chanzo cha mlipuko wa
ugonjwa wa Kipindupindu kilitokana na familia ya Filbert Nchimbi kuanza
kutapika na kuharisha kinyesi cha njano ambapo walipelekwa kituo cha afya
Mbamba bay na kubaini dalili za tatizo hilo.
Pia alisema kuwa mwanafunzi wa miaka
tisa ambaye ni wa darasa la tatu naye alipelekwa katika kituo hicho cha afya
kwa ajili ya kupatiwa matibabu lakini baadaye alifariki dunia.
Kadhalika alisema sababu kuu ya
chanzo cha tatizo hilo katika maeneo hayo kimetokana na watu kunawa mikono
katika chombo kimoja wakati wa kula, baadhi ya nyumba kutokuwa na vyoo na
nyumba nyingine vyoo vilikuwa vimejaa, upungufu wa maji ya bomba, kula chakula
bila kunawa mikono, uwepo wa migahawa ya kuuza chakula bila kufuata kanuni za
usafi.
Dokta Mutahyabarwa aliongeza kuwa sababu
nyingine ni wakulima wa kilimo cha mpunga kujisaidia ovyo katika mashamba yao
na kusababisha mvua zinazonyesha masika hii kutiririsha uchafu kwenye makazi ya
watu na vyanzo vya maji, unywaji wa pombe za kienyeji bila kuzingatia kanuni za
usafi wakiwa katika mazingira machafu na wavuvi kuwa na mazoea ya kujisaidia
katika vyanzo vya maji.
Hata hivyo mwito umetolewa kwa
wananchi wa wilaya ya Nyasa katika kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo wanapaswa kuzingatia
kanuni bora za usafi ili kuweza kunusuru afya za wengine zisiweze kuathiriwa na
Kipindupindu.
No comments:
Post a Comment