Na Mwandishi wetu,
SERIKALI kupitia Sekretarieti yake ya
Maadili hapa nchini, imewataka viongozi wote wa umma kujaza fomu ya tamko la maandishi
ambalo linaorodhesha Mali au Rasilimali wanazomiliki, kabla ya kufikia Desemba
31 mwaka huu.
Rasilimali hizo ni zile
zinazojumuisha mali za mke na mume pamoja na watoto wao ambao wamezidi umri
kuanzia miaka 18 kuwasilisha kwa Kamishna wa maadili, ambapo kwenye tamko hilo
litajumuisha mali na rasilimali za kiongozi husika.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Ibara ya 132 ya 1977 Sekretarieti hiyo ya maadili ya viongozi wa
umma ni idara inayojitegemea chini ya Ofisi ya Rais, ambayo ilianzishwa kwa ajili
ya kusimamia utekelezaji wa sheria ya maadili ya viongozi wa umma namba 13 ya
mwaka 1995.
Akizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es salaam leo, Kamishna wa maadili Jaji mstaafu Harold Nsekela alisema
kuwa Sekretarieti hiyo inatoa wito kwa viongozi wa umma ambao hadi sasa bado
hawajapata fomu, wapitie kwenye tovuti ya www.ethicssecretariat.go.tz ambapo
huko ndipo zinapopatikana fomu za tamko hilo la rasilimali na madeni.
Alisema kuwa baada ya kujaza fomu
hizo kiongozi atatakiwa kuziwasilisha katika Ofisi za Sekretarieti ya maadili
ya viongozi wa umma Dar es salaam au katika Ofisi kanda ya kati Dodoma, kanda
ya ziwa Mwanza na kanda ya nyanda za juu kusini iliyoko mjini Mbeya.
Vilevile viongozi wamekumbushwa kwamba
ni kosa kwa mujibu wa kifungu cha 15 (C) cha Sheria ya Maadili ya Viongozi wa
Umma kwa kiongozi kushindwa kutoa tamko bila sababu ya msingi.
Kwa upande wake Afisa sheria mkuu wa
Sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma, Filotheus Manuca alisema kuwa
katika kipindi cha mwaka jana hapakuwa na kiongozi yeyote ambae alifikishwa
kwenye baraza la maadili na kusema kazi kubwa ya Sekretarieti hiyo ni
kuhakikisha kwamba kila kiongozi wa umma anakuwa mwadilifu.
No comments:
Post a Comment