Na Mwandishi wetu,
Mbinga.
BAADHI ya Wanafunzi wanaosoma shule
ya Sekondari Kiamili iliyopo katika kata ya Kigonsera Halmashauri Wilaya ya
Mbinga Mkoani Ruvuma, wameiomba jamii kuona umuhimu wa kushirikiana na Serikali
yao ya awamu ya tano katika kutatua changamoto zinazoikabili shule hiyo hasa katika
ujenzi miundombinu mbalimbali kama vile mabweni ya kulala wanafunzi.
Shule hiyo ambayo ina watoto zaidi ya
800 wa kidato cha kwanza hadi cha nne, inakabiliwa na changamoto kubwa ya
upungufu wa vyumba vya kulala wanafunzi jambo ambalo limesababisha baadhi ya
wanafunzi wa kike sita kwa nyakati tofauti kupata ujauzito na kukatisha masomo
yao.
Wakizungumza na mwandishi wetu, baadhi
ya wanafunzi waliokutwa shuleni hapo wakiendelea na masomo yao wakati huu wa
likizo walisema kuwa, uhaba wa mabweni ni changamoto kubwa kwao hasa
ikizingatiwa kuwa baadhi yao wanaishi mbali na eneo la shule na hujikuta
wakiingia katika vishawishi vya ngono.
Esta Kinyero ambaye ni mwanafunzi wa
kidato cha tatu alisema kuwa tatizo hilo la kuishi umbali mrefu na mazingira ya
shule, limekuwa likichangia pia baadhi yao kukosa hata muda wa kuhudhuria
vipindi vya masomo shuleni kwa wakati.
Naye Saveria Kitusi aliongeza kuwa
changamoto hiyo ya ukosefu wa mabweni imekuwa ikichangia hata wanafunzi wengine
kujiingiza kwenye vitendo vya kiuhalifu na kutozingatia ipasavyo taaluma
shuleni.
Kwa upande wake Mkuu wa shule ya
Sekondari Kiamili, Frank Kinunda alibainisha kuwa katika kukabiliana na tatizo hilo
halmashauri ya wilaya ya Mbinga imeanza kujenga mabweni mawili kwa ajili ya
wanafunzi wa kiume na wasichana.
Kinunda alisema pamoja na ujenzi huo
wa mabweni unafanyika lakini bado hayatoshelezi mahitaji kwani yatakuwa na
uwezo wa kulaza wanafunzi 46 tu badala ya watoto 98 kwa kila bweni kama ilivyokusudiwa.
Alieleza kuwa tayari wamepokea mifuko
100 ya saruji, nondo bati na misumari kutoka halmashauri ya wilaya hiyo kwa
ajili ya kuendelea na ujenzi huo lakini bado kumekuwa na tatizo la jamii
kutoshiriki kikamilifu kwa kujitolea nguvu zao katika shughuli hizo za ujenzi.
No comments:
Post a Comment