Tuesday, December 26, 2017

MAGUFULI NA MAJALIWA WALIVYOTIKISA BANDARINI



KAMA kuna mashirika au taasisi za Serikali ambazo zilikuwa na wakati mgumu kwa mwaka huu unaomalizika, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) huwezi kuiweka kando.

Ugumu wake haukutokana tu na ziara za kushtukiza zilizofanywa na Rais John Magufuli na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa katika Bandari ya Dar es Salaam, bali yale ambayo viongozi hao wakuu wa nchi waliyabaini; wizi, upigaji dili na ubadhirifu wa mali za umma.

Waliibua zaidi ya matukio matano kwa nyakati tofauti bandarini hapo jambo lililoashiria kuwa kulikuwa na mchezo mchafu uliokuwa ukiendelea katika eneo hilo nyeti kwa uchumi wa nchi.


Mara zote walipofanya ziara, kama si kubaini udanganyifu wa taarifa za uingizwaji mizigo, basi walikumbana na ukwepaji kodi wa bidhaa na mizigo iliyoingizwa hapa nchini.

Miongoni mwa mambo waliyoyabaini ni kuwapo kwa vichwa 13 vya treni visivyo na mwenyewe, magari 53 aina ya Suzuki ambayo ni maalumu kwa ajili ya kubebea wagonjwa yaliyohusishwa na Ofisi ya Rais na malori zaidi ya 50 ya Jeshi la Polisi ambayo yaliingizwa tangu mwaka 2015 bila kuwa na nyaraka zinazoeleweka.

Magari yaingizwa kwa jina la Ikulu.

Novemba 26, Rais Magufuli alifanya ziara bandarini hapo kuwaaga mabaharia wa meli ya Peace Arc kutoka China waliokuwa wakitoa huduma ya matibabu kwa wiki moja, lakini baada ya hafla hiyo fupi alitembelea eneo la maegesho ya magari hayo yanayodaiwa kuingizwa na Ofisi ya Rais.

Akionekana kama wakili anayewabana mashahidi wa upande mwingine, Rais aliuliza maswali kutoka kwa Waziri mmoja hadi mwingine, mtumishi mmoja wa Serikali hadi mwingine akitaka kujua aliyeyaagiza, sababu za taarifa kutotolewa kwa takribani miaka miwili, wahusika kutowafuatilia. 

Katika hili waliowekwa katika hali ngumu ni Dokta Philip Mpango, ambaye ni Waziri wa Fedha na Mipango, Profesa Makame Mbarawa (Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano), Valentino Mlowola (Mkurugenzi Mkuu Takukuru), Simon Sirro (Mkuu wa Jeshi la Polisi), George Mnyitafu (Kaimu Kamishna wa Forodha wa TRA) na Deusdedit Kakoko ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Nchini (TPA).

Wengi walionekana kupata taarifa za magari hayo wakati wa ziara hiyo, kiasi cha kumfanya Rais aonekane kutoridhishwa na utendaji wao wa kutofuatilia vizuri kazi zao na kufanya magari mengine kukaa bandarini kwa takriban miaka 10 wakati sheria inaruhusu siku 21.

“I’m sorry jamani, haya mengine ni frustration zangu, nisameheni sana,” alisema Rais Magufuli baada ya kueleza udhaifu wa utendaji wa vigogo hao wa kutochukua hatua.

Rais, ambaye alisema ana taarifa za magari hayo na mtu aliyeyaagiza, alitoa siku saba kwa mawaziri na wakuu hao wa taasisi wawe wamempa taarifa kamili ya suala hilo.

Kabla ya kutoa maagizo hayo, Rais Magufuli aliwahoji mawaziri na viongozi hao wa taasisi ambao kila mmoja alipewa kipaza sauti ili majibu yake yasikike.
Alianza kwa kumhoji Kakoko kuhusu uhalali wa magari hayo kukaa bandarini kwa muda mrefu na aliyeyaagiza.

Rais Magufuli: Nataka kujua haya magari ni ya nani?

Kakoko: Haya magari yameingia wakati hujaingia madarakani, ila yameingizwa na Ofisi ya Rais. Jina la aliyeyaagiza ni la Kichina au Kihindi hivi, lakini anwani ya mwingizaji ni Ofisi ya Rais ingawa na lenyewe limeandikwa vibaya vibaya na hata maneno yana utofauti. Magari yapo 50.
Rais: Kwa hiyo yameagizwa na ofisi yangu? Kuna mtu yeyote wa ofisi yangu ambaye aliagiza?

Kakoko: Hili jina si la mtu wa ofisini kwako na anuani si ya ofisi yako, bali ni lile jina la mwanzo tu.

Rais: Lakini wanasema yameagizwa na Ofisi ya Rais?
Kakoko: Ndivyo nyaraka zinavyoonyesha.

Rais: Mmeshafanya juhudi gani kama tangu mwaka 2015 Rais ameagiza magari kwa jina la Kichina na hayajachukuliwa na yamekaa hapa kwa jina la Kichina mpaka leo. Ulifanyaje? Ulimjulisha Waziri? Na yeye anasema ndiyo amepata taarifa leo.

Kakoko: Utaratibu wetu baada ya siku 21 huwa unahama kwetu. Kimsingi yanakuwa yamehamia TRA.

Rais: Kamishna wa TRA yupo hapa hebu tueleze kuhusu haya magari ya Rais.

Mnyitafu: Rais ni kweli magari haya yaliingia mwaka 2015 Juni na taratibu zetu za kiforodha ilitakiwa tuyatangaze baada ya siku 21 ili yaweze kuuzwa.
Rais: Mliyatangaza?

Mnyitafu: Bado baada ya kushauriana na uongozi…
Rais: Mlishauriana na uongozi gani? Nataka jibu ndiyo maana nimewaita viongozi wote hapa.

Mnyitafu: Uongozi wa mamlaka wa wakati huo, tukashauriana, lakini sikuwepo wakati huo.

Rais: Nani ulimhusisha kwenye uongozi ule taja tu majina.
Mnyitafu: Sikuwepo.

Rais: Ulijuaje kama walishauriana wakati hukuwepo?
Mnyitafu: Nilivyouliza kwa wenzangu ambao…
Rais: Nani jina lake?

Mnyitafu: Maofisa ambao wapo bandarini.
Rais: Ulimuuliza nani, taja jina lake?

Mnyitafu: Meneja wa bandari ambaye yupo sasa hivi. Hata hivyo yeye ni mgeni anasema aliambiwa.

Rais: Nataka uwe muwazi, wewe si msomi bwana? Mimi mpaka kuja hapa nina taarifa nyingi ndiyo maana nataka uwe wazi ili nijue. Si umemuona mwenzako amesema wazi ofisi yangu ndiyo ilihusika mwaka 2015?

Mnyitafu: Sisi tunaangalia mtu wa kwanza aliyeagiza ambapo inasomeka kama imeagizwa na Ofisi ya Rais.
Rais: Ameshakuja mteja yeyote kufuata magari haya hapa?
Mnyitafu: Hajaja mteja yeyote kuchukua magari haya.

Rais: Ina maana hamjafanya upelelezi wowote kutambua kwamba haya magari ni ya nani?
Mnyitafu: Tuliamini kwamba ni ya Ofisi ya Rais.
Rais: Labda niulize swali jingine. Magari ya polisi yalikuja lini na haya pia yalikuja kipindi gani?

Mnyitafu: Yamekuja mwaka 2015 mwezi Juni.
Rais: Ndiyo maana nauliza magari ya polisi yalikuja mwezi wa sita na haya ya mtu ambaye hajulikani yamekuja Juni huyu hajayachukua? Polisi magari yenu yapo mangapi?

IGP Sirro: Yapo 55.
Rais: Sirro, haya magari 50 ambayo ni ambulance yanawahusu ninyi?
IGP Sirro: Hapana kwa kweli hatuyatambui na hatujui chochote kuhusu magari haya.

Rais: Nani mwingine anayefahamu kuhusu haya magari? Waziri pia hujui chochote.
Profesa Mbarawa: Mimi sijui. Nimepata taarifa leo asubuhi.

Rais: Kwa hiyo tangu mwaka 2015 Juni aliyekuwa mkurugenzi wa pale TPA mpaka ameondoka ndugu (Madeni) Kipande hakutoa taarifa na aliyeingia naye hakutoa taarifa na wewe waziri watu wako wa TRA waliokuwepo na walioko mpaka sasa hivi hawajaeleza kuwa kuna magari hamsini na kitu ambayo yamekaa hapo kwa miaka miwili, ambayo hayana mwenyewe, yameandikwa hapa president’s office wala hata mimi sijaulizwa. Mtu wa PCB, hebu njoo hapa wewe unafahamu kuhusu hili kwa sababu wewe ndiyo mtumiaji na mpelelezi mzuri. Unafahamu chochote kuhusu haya magari?

Mlowola: Kwa sasa sijui chochote mheshimiwa Rais. Ndiyo kwanza nimepata taarifa hii.
Rais: Na wewe ndiyo umepata taarifa hii leo kwa hiyo mtu wako wa PCB anayekaa bandarini naye hajui? Sheria za TRA zinasemaje Mheshimiwa Waziri? Gari linaweza likakaa humu hata miaka 30 mnatunza tu?

Waziri Mpango: Hapana mheshimiwa Rais. Sheria zinaweka ukomo wa muda na baada ya hapo inabidi zinadiwe.
Rais: Sasa kwa nini haya hayajanadiwa wala hayajatangazwa mnada kuanzia mwaka 2015?

Waziri Mpango: Kwa kweli kama nilivyosema sijui labda kamishna wa customs (ushuru) anisaidie kwa idhini yako.
Rais: Kamishna wa customs (ushuru) kwa nini hayajanadiwa au ulipewa rushwa kusudi usinadi ili kusudi siku tutakapokuwa tunatoa magari ya Serikali na haya yatoke?

Kamishna wa Forodha: Hapana mheshimiwa kama nilivyosema kwamba haya magari yaliandikwa ofisi ya Rais na siyo ofisi ya Rais tu kwa Serikali.
Rais: Kwa nini hukuandika barua kuuliza ofisi ya Rais, na Rais yupo.
Mnyitafu: Mheshimiwa tumeunda kikosi kazi kwa sababu ya kupitia magari haya pamoja na mengine. Mengi ambayo yapo bandarini ni matatizo kama haya.

Rais: Kwa hiyo yako magari mengi yaliyoandikwa Ofisi ya Rais.
Mnyitafu: Hapana, magari ambayo yamepitiliza muda wa kukaa bandarini lakini hayajauzwa.
Rais: Magari ya polisi yamebaki mangapi?
Mnyitafu: Ninayoyafahamu yapo 32 yapo 28 na mengine manne.
Rais: Wewe unayafahamu mangapi?

Kakoko: Yapo ya awamu tatu, ambayo hayajachukuliwa, yaliyochukuliwa zamani, lakini hayo ambayo wamesema wanagawiwa ya awamu tatu yapo kadri 53.

Jina la Waziri Mkuu latumika

Novemba 29 ikiwa ni siku tatu baada ya ziara ya Rais, Waziri Mkuu Majaliwa naye alifika bandarini hapo na kubaini uwapo wa matrela 44 yaliyotaka kutolewa bandarini kwa jina lake.
Tukio hilo lilisababisha kutimuliwa kazi kwa maofisa kadhaa akiwamo aliyekuwa Mkurugenzi wa Ulinzi na Naibu Mkurugenzi Mkuu, Lazaro Twange.
Pia, Majaliwa alimuagiza IGP Sirro kumkamata wakala wa kampuni ya Wallmark anayefahamika kwa jina la Samwel na mfanyabiashara anayefahamika kwa jina la Bahman kutoka kampuni ya NAS kwa tuhuma za kutaka kutoa bandarini magari makubwa 44 ‘semi trailers’
kutoka katika kampuni ya Serini ya Uturuki bila kulipa kodi kwa kutumia jina la Waziri Mkuu.
Pia, aliitaka TPA kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na kutowasikiliza wafanyabiashara wanaotaka kukwepa kodi kwa madai ya kupewa vibali vya msamaha kutoka kwa viongozi wa juu serikalini.
“Mtu asije hapa aseme amepewa kibali na Rais, Makamu wa Rais au Waziri Mkuu cha kutaka kutoa mzigo wake bila ya kufuata taratibu. Akija mtu na taarifa hizo akamatwe mara moja na achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria,” alisema.
Waziri Majaliwa alisema Bahman wa kampuni ya NAS alitaka kupata msamaha wa kodi kwa kuidanganya TPA kwa madai kwamba wamewasiliana na Waziri Mkuu na wasipotekeleza jambo hilo watapata matatizo.
Waziri Mkuu alifafanua kuwa mfanyabiashara huyo alitaka kuyatoa matrela hayo bila ya kukamilisha malipo ya ununuzi kutoka kampuni ya Serin ya Uturuki.
“Magari haya aliyalipia asilimia 30 tu kwa makubaliano ya kumaliza asilimia 70 iliyobaki baada ya kufika Tanzania na atakapokamilisha ndipo angepewa nyaraka, ambayo inaonyesha jina la mwenye mzigo, aina ya mzigo na thamani (bill of lading) inasaidia mteja kufanyiwa tathmini ya gharama za kulipia ushuru, lakini huyu bwana hajafanya hivyo,” alisema.
Alieleza kuwa kitendo cha kuyasajili magari hayo bila ya kuwa na nyaraka hizo, ni kinyume cha sheria; na pia kinaweza kusababisha kampuni iliyouza magari hayo ya Serin kutolipwa malipo yaliyobaki.
Alisema jambo hilo halikubaliki kwa sababu linaweza kudhoofisha uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Uturuki, kwani tayari kampuni hiyo imeshawasilisha malalamiko katika ofisi za Ubalozi wa Uturuki nchini.

Vichwa vya treni vyakosa mwenyewe

Julai 2, Rais Magufuli alishikwa na mshangao baada kukuta vichwa 13 vya treni vikiwa vimeshushwa bandarini lakini havijulikani ni vya nani. Alikumbana na hali hiyo alipokwenda kuweka jiwe la msingi katika mradi wa upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam.
“Kuna vichwa 13 vya treni vilishushwa hapa lakini havina mwenyewe. Inawezekana vipi vichwa vya treni vinafika hapa bandarini, vinashushwa lakini mwenyewe hajulikani! Ni kwa sababu hakuna ‘coordination’, huo ni mchezo mchafu. Vyombo vya dola vianze kuwachunguza hao,” alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli aliendelea kuhoji, kwa nini wahusika hawakuuliza ni vya nani tangu awali ila baada ya meli kuondoka ndipo waulize! “Siku nyingine si watakuja kushusha hata na vifaru au makontena ya sumu,?” alihoji.
Kutoka na hilo, Wizara ya Uchukuzi na Mawasiliano iliiagiza TPA na TRA kuandaa taarifa kuhusu vichwa hivyo.

Sakata la makinikia

Machi 23, Rais Magufuli alifanya tena ziara ya kushtukiza katika bandari hiyo akifuatilia utekelezaji wa maelekezo aliyoyatoa kwa nyakati tofauti juu ya kudhibiti udanganyifu wa mizigo inayoingia na kutoka nchini.
Katika ziara hiyo alikuta makontena 20 ya mchanga wenye madini ambayo yalizuiliwa kusafirishwa nje ya nchi tangu alipotoa agizo la kupiga marufuku usafirishaji wa mchanga nje ya nchi Machi 2.
Kutokana na hali hiyo, alimwagiza aliyekuwa IGP, Ernest Mangu na vyombo vingine vya dola kuhakikisha mchanga huo unashikiliwa popote ulipo mpaka hapo uchunguzi wa kina utakapofanyika kubaini ukweli.
Siku mbili baadaye, TPA ilizuia makontena 262 yenye mchanga huo yaliyokuwa kwenye bandari hiyo. Makontena hayo yalikuwa na lakiri (seal) za TRA. Kuzuiwa kwake ndio ukawa mwanzo wa Rais kuunda tume kuchunguza biashara ya madini ambako matokeo yake yalisababisha vigogo kadhaa kung’olewa katika nyadhifa zao sambamba na kubadilishwa kwa sheria za madini.

No comments: