Na Dustan Ndunguru,
Songea.
KADA wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoka
kata ya Butobela, Wilayani Geita Mkoa wa Geita, Robert Nyamaigolo amewataka
wapiga kura katika uchaguzi mdogo unaotarajia kufanyika Januari 13 mwaka huu
katika jimbo la Songea mjini Mkoani Ruvuma, kuhakikisha kwamba wanamchagua
mgombea wa Chama hicho ili aweze kutekeleza ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015 kwa
vitendo.
Pia amewaasa watendaji, viongozi na
wanaCCM kuainisha maeneo ambayo wapinzani walishinda katika uchaguzi wa Serikali
za mtaa uliofanyika mwaka 2014 na kuyapangia mkakati kabambe utakaopelekea
kuyarejesha mikononi mwa chama mwaka 2019.
Nyamaigolo alisema hayo juzi wakati
alipokuwa akizungumza na Waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa
mkutano wa kampeni ya uchaguzi mdogo wa Ubunge uliofanyika viwanja vya Majengo
mjini hapa.
Alisema kuwa tangu kuingia madarakani
kwa Serikali ya awamu ya tano kasi ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi imekuwa
kubwa jambo ambalo wananchi wengi wanaendelea kujenga imani na chama chao.
“Nawasihi wananchi wa Songea mjini
waendelee kukiamini Chama cha mapinduzi na Serikali yake iliyopo madarakani
kwani imekuwa ikiahidi na kutekeleza, hivyo mchagueni Ndumbaro ili aendeleze
pale ambapo mtangulizi wake aliishia”, alisema Nyamaigolo.
Kada huyo kutoka Mkoani Geita alieleza
pia baada ya kufanyika kwa uchaguzi huo kinachotakiwa ni kwa watendaji, viongozi
na wanachama kupanga mikakati ambayo itakivusha chama katika uchaguzi wa Serikali
za mitaa ujao ambapo wenyeviti wa vijiji, vitongoji na mitaa watachaguliwa.
Nyamaigolo alisema jambo la kwanza ni
vyema yakaainishwa vizuri vijiji, mitaa na vitongoji ambavyo vinashikiliwa na
wapinzani ambapo baada ya hapo yaorodheshwe yale ambayo yalisababisha CCM
kushindwa kwenye maeneo hayo na kuyafanyia kazi kwa umakini mkubwa na kwa
wakati ili uchaguzi huo unaokuja yote yarejeshwe mikononi mwa chama
kinachotawala na sio vinginevyo.
Aliongeza kwa kuwataka wanaCCM
kuandaa wagombea wenye sifa na ambao wanakubalika kwa wananchi na kwamba
mabadiliko yaliyofanyika ndani ya chama hususan nyakati za chaguzi nayo
yazingatiwe kwa ustawi wa chama tawala na kwa upande wa wale ambao bado
wataendelea kufanya kazi kwa mazoea wawajibishwe ili iweze kuwa fundisho kwa
wengine.
No comments:
Post a Comment