Na Mwandishi wetu,
Tunduru.
ZOEZI la kutambua watumishi wenye
vyeti feki lililofanywa na Serikali katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi
wa Rais Dokta John Magufuli, limesababisha idara ya afya katika Halmashauri ya wilaya
ya Tunduru mkoani Ruvuma kuwa na upungufu wa watumishi 947 sawa na asilimia 73.7
wa kada mbalimbali ambao wanahitajika kufanya kazi katika vituo vya
kutolea huduma za afya wilayani humo.
Hayo yalisemwa na mganga mkuu wa
wilaya hiyo, Dokta Wendy Robert alipokuwa akizungumza juzi na mwandishi wetu
Ofisini kwake ambapo alisema kada inayoongoza kuwa na upungufu mkubwa ni
maafisa tabibu (CO) kwani mahitaji halisi ni 110 na waliopo ni 10 tu.
Aidha Dokta Robert alieleza kuwa eneo
lingine lenye upungufu ni maafisa tabibu wasaidizi (ACO) madaktari, madaktari
wasaidizi na kwamba huwalazimu waliopo kwa uchache wao kufanya kazi bila
kupumzika ili kuwatendea haki wananchi wanaofika kwa ajili ya kupata
huduma za matibabu.
Dokta Robert aliyataja maeneo mengine
yanayokabiliwa na upungufu huo kuwa ni idara ya meno, famasia, Daktari wa
meno msaidizi (ADO) maafisa wauguzi, wateknolojia wasaidizi, kitengo cha
maabara, mionzi na maafisa afya.
Vilevile katika mwaka 2017/2018 alisema
idara ya afya imepokea watumishi wapya saba kati ya tisa waliopangiwa kufanya
kazi katika halmashauri ya wilaya ya Tunduru, hata hivyo kati ya hao watumishi saba
walioripoti mtumishi mmoja anayo hitilafu ya uwiano wa vyeti na kada
aliyopangiwa.
Dokta Robert alisema licha ya
upungufu huo wa wataalamu na watumishi wa sekta ya afya Serikali inaendelea na
ujenzi wa wodi mbili katika hospitali hiyo ya wilaya na zahanati moja katika
kijiji cha Legezamwendo.
Katika kuunga mkono jitihada hizo
zinazofanywa na Serikali wananchi nao wameanza ujenzi wa kituo cha afya
Nakayaya kwa nguvu zao ili kuweza kuwarahisishia upatikanji wa huduma za afya
jirani na maeneo yao wanayoishi.
Katika hatua nyingine Dokta Robert
alisema idara ya afya katika halmashauri ya wilaya ya Tunduru ina jumla ya
vituo 65 vya kutolea huduma za afya zikiwemo hospitali tatu kati ya hizo moja
ni ya Serikali na mbili za mashirika ya dini, vituo vya afya vitano ambavyo
vyote vinamilikiwa na Serikali na zahanati mbili ambazo zinamilikiwa na watu binafsi.
Alisema kutokana na mpango wa
Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM) unaoelekeza uwepo wa zahanati katika
kila kijiji na kituo cha afya kwa ngazi ya kata, halmashauri hiyo inaendelea
kuimarisha zahanati zake kwa kuwa tayari kila kijiji kina zahanati.
No comments:
Post a Comment