Na Dustan Ndunguru,
Namtumbo.
MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya
wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma, Christopher Kilungu amekamata watu
wakiwa na malori tisa Kampuni ya YARA na katapila moja lililokuwa
likitumika kupakia kokoto kwenye malori hayo, ambazo ni mali ya kijiji cha
Mchomoro kata ya Mchomoro wilayani humo.
Kukamatwa huko katika kijiji
hicho ni baada ya Diwani wa kata hiyo, Kassim Nabeha kupata taarifa
kutoka kwa wananchi wake kuwa kuna magari yanapakia kokoto za
kijiji hicho ambazo zilitolewa kama zawadi kwa kijiji cha Mchomoro na
Kampuni ya China Railway Seventh Group Company Limited (CRSG) iliyokuwa
ikijenga barabara ya lami kutoka Namtumbo mpaka Tunduru.
Nabeha alipofika katika eneo la tukio
na kufanya mahojiano na madereva wa magari hayo ni nani aliyewapatia kibali cha
kupakia kokoto hizo ambapo alipewa majibu ya kubabaisha na hatimaye alilazimika
kuwasiliana na Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Kilungu na hatimaye waliweza
kuchukua hatua.
Mkurugenzi huyo aliweza kuchukua
hatua kwa kutoa taarifa Polisi ambapo waliambatana na kwenda katika eneo la
tukio na kufanikiwa kukamata magari ya Kampuni ya YARA na kuyafikisha Kituo kikuu
cha Polisi wilayani Namtumbo.
Kwa mujibu wa
maelezo ya diwani huyo alimthibitishia Mkurugenzi mtendaji wa wilaya hiyo kuwa
kokoto hizo zilitolewa na Kampuni ya CRSG kwa kijiji cha Mchomoro na kuongeza
kuwa sio kokoto pekee bali walipewa Pampu ya maji ya kisima cha samaki, nyumba
ya bati ya walinzi, mbao na nguzo za kufunga taa za umeme.
Diwani Nabeha alimwambia Mkurugenzi huyo
kuwa mara baada ya kukabidhiwa kokokoto hizo baraza la maendeleo la kata lilipitisha
na kukubaliana kwamba kokoto hizo, zitumike katika ujenzi wa zahanati za
vijiji vya kata ya Mchomoro ambapo hivi sasa kijiji cha Masuguru na Mchomoro wanaendelea
na ujenzi wa zahanati hizo na kwamba kokoto hizo ndio tegemeo katika
kukamilisha kazi ya ujenzi huo.
Msemaji wa madereva waliokuwa
wakiendesha magari hayo ambayo yalikuwa yakipakia kokoto hizo, aliyefahamika
kwa jina moja maarufu la Mndende alisema kuwa wao hawafahamu utaratibu
uliotumika kwenda kuchukua kokoto hizo ambapo wao walipata maelekezo kutoka kwenye
kampuni ya YARA kwenda kupakia kokoto hizo.
Hata hivyo malori hayo
yalipelekwa Kituo cha Polisi wilayani Namtumbo kwa ajili ya kuchunguza kosa la
uvamizi wa kuchukua kokoto za kijiji cha Mchomoro bila idhini ya Serikali ya
kijiji au Ofisi ya Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo.
No comments:
Post a Comment