Afisa mipango wa wilaya ya Mbinga, Onesmo Mapunda. |
Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.
HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbinga
mkoani Ruvuma, imeingia mkataba wa kukopa vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya
shilingi bilioni 1.2 na Kampuni ya Kisarawe Cement Company Limited na M.M Intergrated
Mills Company Limited, ili kuweza kukamilisha ujenzi wa miradi ya maendeleo ya
wananchi vijijini.
Aidha imeelezwa kuwa makampuni hayo
yapo jijini Dar es Salaam na kwamba mpaka sasa vifaa walivyoanza kuchukua baada
ya kuingia mkataba huo ni vya shilingi milioni 462 na kwamba tayari vifaa vya
shilingi milioni 150 vimesambazwa katika miradi ya wananchi wilayani humo.
Afisa Mipango wa halmashauri ya
wilaya hiyo, Onesmo Mapunda alisema hayo juzi alipokuwa akizungumza na
waandishi wa habari Ofisini kwake, juu ya jukumu la halmashauri hiyo kutoa
huduma endelevu za kijamii na kiuchumi kwa wananchi wake.
Mapunda alifafanua kuwa lengo kubwa
la kufanya hivyo ni kuweza kupunguza kero zilizodumu kwa muda mrefu ili
wananchi waweze kupata huduma kwa ukaribu ikiwemo za afya na elimu ili
wanafunzi nao waweze kusoma katika mazingira mazuri.
Alisema kuwa katika wilaya ya Mbinga,
kuna miradi 600 ambayo inahitaji kukamilishwa ujenzi wake na kwamba licha ya
wilaya kuwa na vijiji 121 lakini zahanati ambazo zimekamilika ujenzi huo ni 54
tu.
Kufuatia hali hiyo uongozi wa
halmashauri kwa kushirikiana na Madiwani wake waliona ni vyema waingie mkataba
huo wa kukopa vifaa ili kuweza kufikia malengo husika ya kukamilisha miradi
yote viporo iliyopo wilayani hapa.
Kadhalika alibainisha kuwa miradi
ambayo mpaka sasa imepelekewa vifaa hivyo vijijini kwa wananchi ni ya ujenzi wa
zahanati, ukamilishaji wa vyumba vya maabara, vyumba vya madarasa kwa shule za
msingi na sekondari, nyumba za watumishi pamoja na mabweni ya kulala wanafunzi.
Afisa mipango huyo aliongeza kuwa
miradi 162 iliyopo katika kata 29 za wilaya ya Mbinga, mpaka sasa tayari
imekwisha pelekewa vifaa vya ujenzi ikiwemo bati, saruji, misumari, nondo na
yapo baadhi ya maeneo tokea vifaa hivyo vigawiwe wananchi wameweza kushiriki
kikamilifu katika ujenzi huo.
Pia alibainisha kuwa wanakopa vifaa
hivyo vya ujenzi katika makampuni hayo na hapo baadaye wakipata fedha kutokana
na mapato yao ya ndani watakuwa wakilipa fedha kwa awamu kulingana na makubaliano
husika yaliyopo kwenye mkataba wao.
No comments:
Post a Comment