Na Muhidin Amri,
Tunduru.
HALMASHAURI ya wilaya ya Tunduru
mkoani Ruvuma kwa kushirikiana na bodi ya korosho nchini, imeotesha miche bora
ya zao la korosho 638,000 kwa ajili ya kuwapatia miche hiyo bure wakulima wake
wanaozalisha zao hilo katika maeneo mbalimbali wilayani humo.
Afisa kilimo wa halmashauri hiyo,
Chiza Malando alisema miche hiyo imezalishwa kupitia vikundi vya wakulima
ambavyo vilipatiwa elimu juu ya uzalishaji huo na mwitikio wake katika
utekelezaji wa jambo hilo umekuwa mzuri.
Lengo la kufanya hivyo ni kuweza
kuongeza uzalishaji wa zao hilo ambalo ni tegemeo kubwa kwa kukuza uchumi wa
wananchi wa wilaya hiyo.
Malando alisema, mpango huo ulianza
tangu mwaka 2008 kupitia sekta ya uendelezaji wa kilimo nchini, hata
hivyo bado kulikuwa na mwamko mdogo ambapo kufikia mwaka 2016 waliweza
kuzalisha miche 295,000 na mkakati wa halmashauri hiyo ulikuwa ni kuzalisha miche
658,000 katika ekari 21,000 kwa wakulima hao wa Tunduru.
Kwa mujibu Afisa kilimo huyo
alibainisha kuwa tangu kuanza kwa mkakati huo mwitikio wa wakulima umekuwa mkubwa
ambapo katika kutekeleza hilo miche 295,000 iliyozalishwa mwaka juzi ilionekana
ni michache baada ya mahitaji ya wakulima kuwa makubwa.
Vilevile Malando alionesha
kufurahishwa na uzalishaji wa korosho hizo kwa msimu uliopita ambapo wakulima
wilayani humo waliweza kuzalisha tani 14,700 za zao hilo kiasi ambacho
hakijawahi kufikiwa.
Alisema malengo ya halmashauri ni
kuhakikisha kwamba wakulima wote wanawafikia ili waweze kuendelea kuboresha
uzalishaji na kufikia kiwango bora zaidi cha uzalishaji ambapo wakulima wameanza
kuondoa shambani mikorosho ya zamani na kupanda miche ya kisasa.
Aliwashauri wakulima wa korosho
wilayani Tunduru kutumia vyema fedha wanazopata kwa ajili ya kufanya shughuli
za maendeleo kwa kujenga nyumba bora, kusomesha watoto na kujiepusha na anasa
ili waweze kuondokana na umaskini katika familia zao.
Pia amewataka kutumia fedha hizo kwa
kubuni miradi mingine ya kiuchumi kama vile ufugaji wa ng’ombe, kuku na mbuzi
ambao watasaidia pia kujiongezea kipato chao katika familia.
No comments:
Post a Comment