Thursday, December 13, 2012

KUSHINDWA KUTOA TAARIFA YA MAENDELEO YA WANANCHI NI ISHARA GANI ?

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu.




















Na Kassian Nyandindi,                         Uchambuzi.              

NIMEKUWA nikitafakari kwa kina juu ya tukio lililojitokeza siku kadhaa zilizopita katika ziara ya Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, iliyofanyika hapa wilayani Mbinga na Nyasa mkoani humo.

Tafakari zangu zinaenda sambamba na mkuu wa mkoa huo Said Mwambungu kuwajia juu viongozi wa wilaya hizo, baada ya kushindwa kumuandalia taarifa iliyo katika misingi ya upembuzi yakinifu.

Binafsi namuunga mkono Mwambungu, kwa kuligundua hili mapema na sitakosea nikisema hivi sasa Taifa hili linahitaji viongozi walio makini kama yeye na wenye kupembua mambo kwa haraka, ili tuweze kusonga mbele kimaendeleo.


Kitendo cha uongozi husika, kushindwa kumuandalia kiongozi wa ngazi ya mkoa taarifa inayochambua maendeleo ya wananchi katika sekta mbalimbali, inaashiria nini?

Na je, hili linaleta maana gani kwa mtendaji wa serikali ambaye serikali imekuamini na kukupatia ajira ukatumikie wananchi kwa kufuata misingi ya utawala bora, na leo tunafikia mahali tunashindwa hata kutoa taarifa yakinifu kwa kiongozi ambaye anakuja kukagua utekelezaji wa miradi hiyo ya wananchi?

Hizi ni zama za ukweli na uwazi, tunaficha nini? yatupasa tuwe wazi katika kutoa taarifa zetu na sio viongozi wanapohitaji taarifa za maendeleo ya wananchi tunawapatia ambazo ‘hazijashiba nyama’ za kutosha, yatupasa tubadilike.

Lawama hizi kwa kitendo kilichotokea Mbinga zimwendee nani, kama sio watendaji husika waliopewa dhamana ya kuongoza wanakondoo wa wilaya ya Mbinga, ambao siku zote wamekuwa wakituamini na leo tunawaangusha mbele ya kiongozi wao wa mkoa wa Ruvuma, tuache uzembe tuwajibike ipasavyo”

Idara ya mipango ndio inalojukumu kubwa la kujua maendeleo yote yanayofanywa katika sehemu husika, lakini inashangaza kuona utekelezaji wa shughuli mbalimbali unashindwa kuwasilishwa ipasavyo kwa viongozi wetu, hii ni aibu.!

Katika kuyasemea haya ni vyema tubadilike na tufanye kazi zetu kwa misingi na taratibu zilizowekwa, tuache kufanya kazi kwa mazoea, jamii ya wanambinga na taifa letu kwa ujumla wanatutegemea sisi tulio madarakani katika mambo mbalimbali ya kusukuma mbele maendeleo, hivyo yatupasa kuwa makini.

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma pongezi zikufikie endelea kuchapa kazi, kaza buti wanaruvuma tupo mbele yako, Mungu ibariki Tanzania na mkoa wa Ruvuma kwa ujumla.

Mwandishi anapatikana kwa barua pepe nyandindi2006@yahoo.com au 0762 - 578960.

No comments: