Tuesday, December 11, 2012

UONGOZI WA WILAYA YA MBINGA NA NYASA LAWAMANI, NI BAADA YA MKUU WA MKOA WA RUVUMA KUIKATAA TAARIFA YA MAENDELEO YA WILAYA HIZO

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma(Kushoto) Said Mwambungu, akiwa katika ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Mbinga leo, majira ya saa 3:15 asubuhi wakati alipokuwa akiikataa taarifa ya maendeleo ya wilaya ya Nyasa na Mbinga kutokana na kutoandaliwa kwa misingi ya upembuzi yakinifu. Upande wa kulia aliyevaa suti nyeusi ni mkuu wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga na kati kati ni mkuu wa wilaya ya Nyasa Ernest Kahindi.(Picha na Kassian Nyandindi)

Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.


MKUU wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu, amewajia juu viongozi wa wilaya ya Nyasa na Mbinga kwa kushindwa kuandaa taarifa sahihi za maendeleo ya wilaya hizo.



Sambamba na hilo mkuu huyo wa mkoa amekataa kupokea taarifa ya maendeleo ya wilaya hizo leo, wakati alipokuwa katika ziara yake ya siku nne ya kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo.

Kitendo cha mkuu huyo wa mkoa kukataa taarifa hizo kilijitokeza katika ofisi ya mkuu wa wilaya ya Mbinga, baada ya kusomewa na ofisa mipango wa wilaya hiyo, Seleman Mwamba na kuwapa muda wa nusu saa kuandaa taarifa nyingine kabla hajaanza ziara yake rasmi.


"Taarifa hii hamjaifanyia uchambuzi yakinifu hasa kwa wilaya ya Nyasa, binafsi naomba muwe makini katika kuandaa taarifa zenu, natoa muda wa nusu saa nahitaji taarifa nyingine kabla sijaondoka hapa", alisisitiza.

Mwambungu yupo katika ziara yake ya siku nne ambayo ameianza leo katika wilaya hizo, akipita kukagua miradi mbalimbali ya kimaendeleo iliyotekelezwa kipindi cha mwaka wa fedha 2011 na 2012.

Taarifa aliyosomewa mkuu huyo wa mkoa wa Ruvuma, haichambui vipengele vya sekta ya elimu, afya, barabara na maendeleo mengine yaliyotekelezwa katika wilaya hizo, hivyo inakuwa ni vigumu kwake kujua ni miradi mingapi imetekelezwa na thamani halisi ya fedha zilizotumika katika miradi hiyo.

"Nataka kutoka na taarifa iliyo sahihi ambayo inatakwimu zinazohusu wilaya ya Nyasa na Mbinga, hii inaonesha ni wazembe katika kufanya kazi", alisisitiza Mwambungu.

Kwa ujumla wilaya ya Nyasa hadi sasa tokea ianzishwe inaendesha shughuli zake kwa kutegemea wilaya mama ya Mbinga, hivyo taarifa hiyo ambayo Mwambungu aliikataa kuipokea, ilitokana na kuandaliwa kwa ujumla bila kuainishwa mambo ya msingi ya kimaendeleo yanayohusu wilaya hizo.

Licha ya Mwambungu kuwapa muda wa nusu saa kuandaa taarifa nyingine, viongozi wa wilaya hiyo walishindwa kuiwasilisha kwake kwa muda aliowapa, ambapo mkuu huyo wa mkoa, alichukua jukumu la kuendelea na ziara yake kwa kuanzia wilaya ya Nyasa, huku akisisitiza taarifa hiyo aipate haraka iwezekanavyo ikiwa imeandaliwa katika uchambuzi yakinifu.

No comments: