Wednesday, December 5, 2012

WANAOWAPA MIMBA WANAFUNZI KUKIONA CHA MOTO

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu.
















Na Steven Augustino,
Songea.

SERIKALI mkoani Ruvuma imeamua kuanzisha kampeni maalumu ya kukabiliana na wahusika wa vitendo vya kuwapa mamba wanafunzi kwa kutoa agizo kwa viongozi wa wilaya na halmashauri zote zilizopo mkoani humo.

Hizo ni juhudi zake kuhakikisha kuwa inakomesha wimbi kubwa la upataji wa mimba kwa watoto wakike wanaosoma katika shule za msingi na sekondari.

Kampeni hiyo inawahamasisha wananchi kuwabaini wanaume ambao wamekuwa wakiwashawishi watoto wa kike  na kuwaharibia mfumo wa masomo na maisha   yao.

Hayo yalisemwa na mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu alipokuwa akizungumza katika kikao cha kamati ya ushauri cha mkoa wa Ruvuma, kilichoketi hivi karibuni katika ukumbi wa Songea Club mjini hapa, ambapo pamoja na mambo mengine aliwaagiza wakuu wa wilaya na wakurugenzi watendaji wa halmashauri pamoja na viongozi wengine kuhakikisha wanaweka mikakati ya kukabiliana na tatizo hilo ambalo linazidi kuongezeka siku hadi siku mkoani humo.


Mwambungu alisema kuwa hali hiyo inatokana na baadhi ya wahusika wanaofanya vitendo vya kufanya mapenzi na watoto wa shule, miongoni mwao ni watu wazima huku baadhi yao wakiwa ni viongozi wa serikali na taasisi za umma ambao siyo waadilifu.

Aidha aliwataka viongozi kuwa na utamaduni wa kutoa namba zao za simu wazi kwa wananchi na kuwa na tabia ya kupokea wao wenyewe simu zao zinapopigwa ili waweze kufanyia kazi mara moja taarifa na kero zinazotolewa na wananchi.

Aliwataka viongozi kushirikiana na wananchi kukabiliana na tatizo hilo ambalo linawafanya watoto wa kike kushindwa kuhitimu elimu ya msingi au sekondari ikiwa ni pamoja na kutofanya vizuri katika masomo yao kwa sababu ya vishawishi vya watu wenye fedha huku baadhi wakiishia kupata mimba na maradhi kama vile Ukimwi.

Katika hatua nyingine mkuu huyo wa mkoa aliwataka viongozi kuwaelimisha wananchi kushiriki katika kampeni hiyo kwa kutoa taarifa za ukweli na siyo za chuki kwa sababu baadhi ya wananchi wanaweza kuwa na chuki binafsi na baadhi ya watu wakaamua kutoa taarifa za uongo kwa lengo la kukomoa au kudhalilishana miongoni mwao.

No comments: