Sunday, April 8, 2018

BUSTANI MANISPAA SONGEA KUANZA KUTUMIKA MWEZI UJAO


Mandhari ya bustani ya Manispaa Songea Mkoani Ruvuma.

Na Kassian Nyandindi,     
Songea.

MRADI wa bustani ya Manispaa ya Songea uliopo Mkoani Ruvuma, umekamilika na kwamba unatarajia kuanza kufanya kazi mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu, ambapo Mkandarasi husika tayari amekabidhi mradi huo kwa uongozi wa Manispaa hiyo.

Kaimu Mkuu wa idara ya ujenzi wa Manispaa hiyo, Mhandisi Nicolous Danda alisema kuwa mradi huo ulikamilika tangu mwezi Desemba mwaka 2017 huku Mkandarasi aliyepewa jukumu la ujenzi wa bustani hiyo akipewa matazamio ya miezi sita ya ujenzi wa mradi huo ambayo inaishia mwezi Aprili mwaka huu.

Danda amezitaja kazi zilizosalia katika mradi huo kuwa ni kuendelea kuotesha nyasi, kufunga mfumo wa maji taka ambayo inafanywa na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (SOUWASA) na kuweka nishati ya Umeme kazi ambazo zinatarajia kukamilika mapema mwezi huu.


“Wakati wowote kuanzia sasa tunatarajia kitengo cha manunuzi kutangaza zabuni, hivyo hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Mei mwaka huu tunatarajia bustani kuanza kazi’’, alisema Mhandisi Danda.

Kwa ujumla mradi huo umefadhiliwa na Benki ya dunia kwa gharama ya Shilingi milioni 399 na kwamba mradi huo hadi kukamilika kwake umetumia Shilingi milioni 444, fedha zote ikiwa ni za mradi wa Benki hiyo.
Wawakilishi wa Benki ya dunia wameukagua mradi huo na kuridhishwa na kiwango cha ujenzi uliofanyika wa bustani hiyo ambayo inavutia wengi kwa kuwa imebadilisha muonekano wa Mji wa Songea. 

Mradi huo unaofadhiliwa na Benki hiyo chini ya Mpango wa Kuzijengea Uwezo Serikali za Mitaa (ULGSP) una eneo la mgahawa, choo cha kulipia, uzio, maeneo ya kupaki magari (Parking bay), eneo la kupumzikia (Resting huts), maeneo ya kuchezea watoto na inatarajia kuwa na Kituo cha kutolea habari za utalii na uwekezaji za Manispaa na Mkoa wa Ruvuma.

No comments: