Saturday, April 7, 2018

TASAF YAWEZESHA TUWEMACHO TUNDURU UJENZI BWAWA LA MAJI


Na Muhidin Amri,      
Tunduru.

WANANCHI wa Kijiji cha Tuwemacho kata ya Tuwemacho Wilaya ya Tunduru Mkoa wa Ruvuma kwa kushirikiana na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) hapa nchini, wamefanikiwa kujenga bwawa kubwa la maji safi ili kuweza kumaliza kero ya muda mrefu  ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama.

Kuchimbwa kwa bwawa hilo, kumekuja baada ya vyanzo vya maji vilivyopo kwenye kijiji hicho kushindwa kukidhi mahitaji halisi ya wananchi husika, kutokana na ongezeko kubwa la wageni wanaofika kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwemo kilimo cha zao maarufu la korosho.

Afisa Mtendaji wa kijiji cha Tuwemacho, Ali Fadhil alisema kuwa TASAF kupitia mpango wa kunusuru kaya maskini katika kijiji hicho, umewezesha kupatikana kwa majawabu mengi ya kero za wananchi ikiwemo ukosefu wa huduma ya maji.


“Tulikuwa na tatizo kubwa la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, lakini kupitia miradi shirikishi tuliamua kuboresha visima vya asili vya maji pamoja na kuhifadhi vyanzo vya maji kwa kupanda miti ambayo ni rafiki ya maji”, alisema Fadhil.

Katika mkutano uliofanyika kijijini hapo, kwa nyakati tofauti ilielezwa kuwa hali ya upatikanaji wa maji bado imekuwa ni tatizo kwa wananchi hao hivyo kuna kila sababu ya kuendelea kutengeneza ubunifu wa vyanzo vipya vya maji, ambavyo vitaweza kuendelea kusaidia wananchi katika maisha yao ya kila siku.

Wananchi walisema katika mkutano huo kwamba wamekubaliana kuchangia kiasi cha shilingi 2,500 kwa kila kaya ikiwa ni hatua ya kuanzisha ujenzi wa miundombinu ya maji na fedha zilizokusanywa hadi kufikia Machi 20 mwaka huu zimefikia Shilingi milioni 1,500,000.

Fedha hizo imeelezwa kuwa zitatumika kununulia vifaa kama vile mabomba pamoja na pampu za kusukumia maji kutoka kwenye chanzo na kwamba michango hiyo bado inaendelea kuchangishwa ili kuweza kupata fedha zitakazotosheleza kutekeleza mradi huo wa maji.

No comments: