Tuesday, April 24, 2018

UKOSEFU WA GARI CHANGAMOTO INAYOKWAMISHA UTENDAJI KAZI KITENGO CHA UZAZI NA MTOTO MBINGA

Baadhi ya Wananchi waliokusanyika jana mjini hapa katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga Mkoani Ruvuma, siku ya uzinduzi wa chanjo ya kuzuia Saratani ya mlango wa shingo ya kizazi kwa wasichana wenye umri wa miaka 14.

Na Kassian Nyandindi,     
Mbinga.

UKOSEFU wa gari maalum la kusambazia chanjo na vifaa tiba vya kutolea huduma, imeelezwa kuwa ni changamoto kubwa inayoikabili idara ya afya kitengo cha huduma ya afya ya uzazi na mtoto katika vituo vya afya, vilivyopo Halmashauri ya Mji wa Mbinga Mkoani Ruvuma.

Kufuatia uwepo wa tatizo hilo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeombwa kumaliza kero hiyo ndani ya Halmashauri hiyo ili kuweza kuleta ufanisi mzuri wa utendaji kazi kwa idara hiyo katika jamii.

Hayo yalisemwa na Muuguzi wa afya Hospitali ya Halmashauri ya Mji Mbinga, Verena Mapunda alipokuwa akisoma risala ya uzinduzi wa wiki ya chanjo duniani kwa Halmashauri ya Mji huo uliofanyika mjini hapa.


Uzinduzi huo ulifanywa na Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Cosmas Nshenye ambapo katika kuadhimisha wiki hiyo kutakuwa na uanzishwaji wa chanjo ya kuzuia Saratani ya mlango wa shingo ya kizazi kwa wasichana wenye umri wa miaka 9 hadi 14 (Human Papiloma Virus) ambayo itatolewa sambamba na chanjo nyingingine ya ziada inayokinga ugonjwa wa Polio.

Mapunda alifafanua kuwa zoezi hilo linalenga pia utoaji wa elimu endelevu kwa jamii ili iweze kutambua umuhimu wa chanjo kwa watoto wao na kuweza kuhamasika kushiriki kikamilifu katika kuhakikisha kwamba wanapata chanjo kwa wakati kulingana na ratiba iliyopangwa.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo, Nshenye alisisitiza kuwa katika kuzingatia kauli mbiu ya siku ya chanjo duniani isemayo, Jamii iliyopata chanjo ni jamii yenye afya timiza wajibu wako, wananchi sasa wanapaswa kujitokeza kwa wingi kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo ili kuwezesha kuwa na jamii imara na madhubuti kiafya ambayo haishambuliwi na magonjwa kwa urahisi.

Pia Nshenye amewataka viongozi wa Mji huo kuhimiza jamii kwa kutoa elimu endelevu kuhusu chanjo hiyo ili wazazi waweze kupeleka watoto wao katika vituo vya kutolea huduma ya afya.

Hata hivyo Mji wa Mbinga katika utekelezaji wa zoezi hili wanatarajia kuwafikia watoto 1,326 kwa wale wasiopata chanjo, ili waweze kupewa huduma husika na hatimaye waepukane na magonjwa yanayoweza kuathiri afya zao hapo baadaye.

No comments: