Sunday, April 8, 2018

WACHINA WAANZA UJENZI STENDI MPYA MANISPAA SONGEA


Wataalamu wa Kampuni ya kichini ya SIETCO wakiwa pamoja na Kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Songea, katika eneo la ujenzi wa Stendi mpya ya mabasi ya abiria ambayo ujenzi wake tayari umekwisha anza. 

Na Kassian Nyandindi,   
Songea.

HATIMAYE Kampuni ya Serikali kutoka nchi ya China inayofahamika kwa jina la, China Sichuan International Cooperation (SIETCO) imewasili mjini Songea tayari kwa kuanza kazi ya ujenzi wa Stendi mpya ya kisasa kwa ajili ya magari ya abiria, katika eneo la Kata ya Tanga Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma.

SIETCO imesaini mkataba wa miezi 18 kwa ajili ya kazi ya ujenzi huo na Halmashauri ya Manispaa hiyo, kujenga Stendi mpya ya mabasi katika eneo hilo la Tanga kuanzia Aprili Mosi mwaka huu.

Mwakilishi wa Kampuni hiyo ameiambia Kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Songea kuwa, wanatarajia kutoa ajira kwa wakazi wa Songea ambapo hivi sasa tayari wametoa ajira kwa wafanyakazi wachache katika hatua za awali kwa ajili ya kuweza kuanza kazi za mradi huo.


Kamati hiyo ikiongozwa na Mwenyekiti wake ambaye ni Mkuu wa Wilaya Songea, Pololet Mgema wamefanya ziara ya ukaguzi wa eneo hilo la ujenzi wa stendi ambapo wamemkuta Mkandarasi akiendelea kufanya maandalizi ya awali ya ujenzi.

Kaimu Mhandisi wa ujenzi katika Manispaa hiyo Mhandisi Nicolous Danda alisema kuwa Kampuni ya SIETCO imesaini mkataba ambao unaanzia Machi 25 hadi Septemba 30 mwaka 2019.

Alisema kuwa mradi hadi kukamilika kwake utagharimu Shilingi bilioni 12 ambapo katika awamu ya kwanza, zitatumika shilingi bilioni sita na kwamba Stendi hiyo inatarajia kuanza kazi baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ya utekelezaji ambayo ni kuanzia Oktoba mwaka 2019.

“Ili kuendana na kasi ya ukuaji wa Mji, Manispaa iliamua kutenga eneo la kujenga Kituo kikuu cha mabasi kuwa Kata ya Tanga ikiwa ni umbali wa takribani kilometa 14 toka mjini Songea’’, alisema Mhandisi Danda.

Vilevile anazitaja kazi ambazo zitafanyika katika awamu ya kwanza na pili ya mradi huo kuwa ni kujenga barabara za kuingia na kutoka stendi zenye kiwango cha lami nzito, kujenga mirefeji ambayo itapeleka maji mtoni, ujenzi wa eneo la stendi lenye ukubwa wa meta za mraba 32,914, kuweka taa za barabarani katika eneo lote la stendi, eneo la utawala na kujenga majengo yenye hoteli za kisasa,

“Fedha za mradi huu wa stendi zimetolewa kupitia Benki ya dunia, jumla ya hekari 15 zimetwaliwa katika eneo hili ili kupitisha stendi ambapo Shilingi milioni 32 tayari zimelipwa kama fidia kwa wananchi waliokuwa katika eneo hili’’, alisema Mhandisi Danda.

Kampuni ya SIETCO imesaini pia mkataba wa miezi 18 wa ukarabati wa barabara za lami nzito katika Manispaa ya Songea, zenye urefu wa kilometa 10.3 kwa thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 10 ambapo mkataba huo umeanzia Machi 25 mwaka huu hadi Septemba 30 mwaka 2019.

Fedha za miradi hiyo ya barabara na stendi zimetolewa na Benki ya dunia chini ya Mpango wa Kuzijengea uwezo Serikali za Mitaa (ULGSP), mpango ambao unakusudia kuendeleza miundombinu ya Halmashauri za Miji na Manispaa 18 za Tanzania bara ikiwemo Manispaa ya Songea.

No comments: