Wednesday, April 18, 2018

POLEPOLE ATAKA VIONGOZI WANAOPOTOSHA UMMA WACHUKULIWE HATUA


Na Mwandishi wetu,

KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Itikadi na Uenezi Chama Cha Mapinduzi (CCM) Humphrey PolePole, amefunguka na kuwavaa viongozi ambao wanazungumza juu ya ripoti ya CAG na kusema baadhi ya viongozi hao wanapotosha umma kwa kusema mambo ya uongo.
Humphrey Polepole.

Polepole alisema hayo leo wakati akizungumza na Waandishi wa habari na kusema kuwa wapo viongozi wa vyama vya siasa hawazungumzi juu ya mambo mazuri, yaliyofanywa na Serikali kama vile ujenzi wa miundombinu na mambo wanayopiga hatua ila wamekuwa wakidakia mambo na kutoa taarifa zisizokuwa na ukweli.

“Sasa unaposoma taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) halafu unatoa kauli timilifu kuwa pesa imeibwa, yaani pesa ya umma imeibwa,


“Tunaweza tukakwambia tusaidie kuthibitisha sasa ukishindwa umesema uongo umeuhadaa umma, umetoa takwimu za uongo ukichukuliwa hatua sio ndiyo utaanza kusema uongozi huu hatuna huruma, huruma kwa watu waovu? waongo wanaopotosha kwa makusudi hilo halikubaliki”, alisema Polepole.

Aliendelea kueleza kuwa, “Mimi sielewi huyu anayekwenda mbele kusema taarifa za uongo uongo hivi, ndiyo mtaji wake siku hizi anatafuta tu pahala hoja hana, hazungumzi kuhusu rushwa siku hizi hazungumzi kuhusu huduma za kijamii, hazungumzi kuhusu ufisadi, hazungumzi kuhusu miundombinu, tunapiga hatua kubwa, tunapeleka watoto shule bure, bali yeye anatafuta hoja ya uongo uongo”, alisema.

Polepole katika mkutano huo aliendelea kumtuhumu mtu huyo kushindwa kuwa na uhakiki wa maneno yake.

“Kuna kipindi mtu huyu alizungumza kuhusu njaa, wewe unaijua njaa inatangazwa vipi sasa tumevumilia sana leo tumeshindwa tumeona tumsaidie kumuelewesha halafu tuseme wale ambao wana dhamana ya kuhakiki maneno tunayatoa, kwa kweli wachukue hatua kwani hatupo tayari kuacha watu wachache waendelee kuudanganya umma wa Watanzania hili halikubaliki”, alisisitiza.

Pamoja na mambo mengine, mwishoni mwa wiki iliyopita Mbunge wa Kigoma Mjini kwa tiketi ya ACT Wazalendo, Zitto Kabwe alizungumzia kwa mapana zaidi taarifa ya CAG na kuonyesha mambo ambayo Serikali imetuhumiwa kufanya ikiwa pamoja na upotevu wa fedha zaidi ya trilioni 1.5 ambayo haina maelezo imetumikaje.

No comments: