Friday, April 6, 2018

TUWASA TUNDURU YAONGEZA MTANDAO HUDUMA MAJI SAFI NA SALAMA


Na Mwandishi wetu,     
Tunduru.

IDADI ya Wananchi wanaopata huduma ya maji safi na salama katika Mji wa Tunduru Mkoani Ruvuma, imeongezeka kutoka 23,200 mwaka 2016/2017 hadi kufikia wananchi 32,200 katika kipindi cha mwaka huu.

Aidha kutokana na maboresho ya mitambo na vyanzo vya maji yanayoendelea kufanywa na Mamlaka  ya Maji safi na Usafi wa Mazingira katika Mji wa Tunduru (TUWASA) hivi sasa mgawo wa maji umepungua kwa baadhi ya maeneo ikiwemo Jeshi la magereza, Hospitali ya Wilaya, kambi ya Polisi na maeneo mengine katika mji huo.

Hayo yalisemwa na Meneja wa Mamlaka hiyo, Christopher Mbunda wakati alipokuwa akizungumza na mwandishi wetu mjini hapa, ambapo  alisema TUWASA imeweza kuwa na wateja 1,590 na kati ya hao waliofungiwa mita ni 1,460 na wasio na mita ni 130.


Alisema kuwa wanatarajia kumaliza kuwafungia mita wateja wote waliobakia ifikapo Desemba mwaka huu, hatua ambayo itasaidia kuongeza mapato ya Mamlaka hiyo.

Kwa ujumla mahitaji ya maji kwa kwa siku kwa wakazi wa Mji wa Tunduru ni lita milioni 2,919,420 lakini wananchi wanaopata huduma ya maji safi na salama ni 32,200 sawa na asilimia 66  na kwamba wananchi waliounganishwa kwenye bomba kuu la kusambaza maji hayo ni 1,514. 

Mbunda alieleza kuwa uzalishaji wa maji kwa siku umeongezeka kutoka lita 1,500,000 hadi kufikia lita 1,968,000 hivyo hali ya uzalishaji wa maji kwa sasa hufikia asilimia 67 kutoka asilimia 54 ya mwaka 2016/2017.

Miundombinu ya maji iliyopo Tunduru mjini ilijengwa tangu mwaka 1,953 hivi sasa imechakaa jambo ambalo linasababisha mtandao wa bomba la kusambazia maji kutofika maeneo mapya ya mji, hivyo baadhi ya maeneo kukosa huduma na kulazimika kutumia maji ya kisima.

Aliongeza kuwa licha ya mafaniko hayo bado kuna changamoto kubwa zinazoikabili Mamlaka hiyo ikiwemo uchakavu wa miundombinu ya maji, gharama kubwa ya umeme kwa ajili ya kuendeshea mitambo ya kuzalisha maji, pamoja na baadhi ya taasisi za Serikali kutolipa ankara za maji kwa wakati.

Katika kukabiliana na changamoto hizo Mbunda alisema wameomba fedha kutoka Wizara ya maji Shilingi milioni 300 kwa ajili ya kukarabati na kuongeza mtandao wa maji huku akiliomba Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kusaidia kurekebisha mfumo wa umeme hasa kwenye mitambo ya kusukumia maji.

No comments: