Sunday, April 29, 2018

WATAKIWA KUJIEPUSHA NA MADAWA YA KULEVYA

Mkurugenzi msaidizi wa Kituo cha kulelea watoto Yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi cha Mwangaza mjini Songea Mkoani Ruvuma, Anna Mugenya akiwa amebeba mtoto mchanga ambaye ni wa mwezi mmoja tokea azaliwe ambapo hulelewa kituoni hapo mara baada ya mama yake kufariki dunia alipokuwa amejifungua mtoto huyo.
Na Kassian Nyandindi,  
Songea.

WATOTO yatima na wale wanaoishi katika mazingira hatarishi Wilayani Songea Mkoa wa Ruvuma, wametakiwa kujiepusha na vitendo viovu vya matumizi ya dawa za kulevya ili wasiweze kuharibu afya zao.

Aidha watoto hao wameaswa kujiepusha na wanaume walaghai ambao wanaweza kuwapotezea ndoto za maisha yao ya baadaye, badala yake wanapaswa kusoma kwa bidii na kuwa viongozi wazuri wa kuliongoza taifa hili.

Mgema alisema hayo juzi alipokuwa kwenye hafla fupi ya kuwaaga watoto hao katika kituo cha Mwangaza, ambao wamefikia ukomo wa kuishi kituoni hapo huku akitoa pongezi kwa uongozi wa kituo kwa kuwasomesha hadi kufikia ngazi ya vyuo vikuu.


Alisema kuwa kitendo hicho kilichofanywa ni cha mfano wa kuigwa kwani kumekuwa na baadhi ya watu wakianzisha asasi, kwa lengo la kusaidia watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi lakini mara baada ya kupata ufadhili huwageuza watoto hao kama kitega uchumi cha kunufaisha matumbo yao.

Pia Vermunda Njawike awali akizungumza kwa niaba ya watoto wenzake alisema kuwa wanaushukuru uongozi wa kituo kwa kuwapatia huduma ya chakula, mavazi, malazi, afya na elimu huku akiwataka watoto wenzake kuendelea kuishi katika maadili mema na kuzingatia masomo darasani.

Kwa upande wake Mkurugenzi msaidizi wa kituo hicho, Anna Mugenya ameitaka jamii kuacha tabia ya ubinafsi na badala yake wajenge utamaduni wa kujitoa katika kusaidia watoto yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi, huku akieleza kuwa jukumu la kuwalea watoto hao ni kila mtu.

Aliyataja mafanikio mbalimbali yaliyotokana na kuwasomesha watoto hao ni pamoja na baadhi yao kujiunga na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na wengine kuajiriwa pamoja na kujiendeleza katika fani mbalimbali.

Kituo cha Mwangaza kimekuwa kikipata ufadhili wa kulea watoto hao kutoka nchi ya Japan na Marekani na kwamba wameweza kupata mafanikio mengine, kwa kuendelea kujenga makazi ya kudumu ya kituo hicho katika eneo la Mwengemshindo hapa mjini Songea ikiwemo pia jengo la kulelea watoto wachanga.

No comments: