Monday, April 30, 2018

SERIKALI YAOMBWA KUBORESHA SEKTA YA MICHEZO HAPA NCHINI

Kutoka upande wa kulia aliyesimama ni Mkufunzi wa Mafunzo ya maboresho ya sheria mpya za mpira wa Pete, Yovin Mapunda ambaye ni mwalimu wa Shule ya sekondari Hagati Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma, akiwapatia ujuzi baadhi ya walimu wenzake wa Shule za msingi na sekondari katika ukumbi wa Shule ya Sekondari Mbinga Mkoani humo, juu ya mabadiliko ya sheria mpya za mpira wa Pete ambapo awali Mapunda alipelekwa Zanzibar kwenye mafunzo hayo ili baadaye aweze kutoa elimu hiyo kwa walimu wengine wanaoendesha michezo mashuleni.

Na Kassian Nyandindi,     
Mbinga.

SERIKALI hapa nchini imeombwa kuboresha sekta ya michezo hasa kwa mpira wa Pete, ili kuweza kuongeza na kuimarisha vipaji vya wachezaji wa mpira huo na kulifanya Taifa liweze kusonga mbele katika michezo.

Aidha Serikali kupitia Waziri wake wa habari, utamaduni, sanaa na michezo Dkt. Harrison Mwakyembe imeombwa kubadilisha mfumo wa uendeshaji wa michezo katika Shule za msingi na sekondari ili kuweza kuleta mabadiliko yenye tija.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Walimu wa Shule za msingi na Sekondari ambao walishiriki wa mafunzo ya siku tatu, ya maboresho ya sheria mpya za mpira wa pete, yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Shule ya sekondari Mbinga iliyopo hapa Mkoani Ruvuma.


Walisema kuwa katika kuimarisha sekta ya michezo ni vyema sasa kuandaa timu za michezo katika mfumo wa Academy, ambao muda wote watoto shuleni wataweza kujifunza jambo ambalo litasaidia hata kuweza kukuza vipaji na viwango vya uchezaji wa michezo hususan kwa mpira wa pete na kuweza kufika mbali zaidi.  

“Serikali yenyewe imekuwa ikitumia Umoja wa Michezo Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) na ule wa Shule za Sekondari Tanzania (UMISSETA) kama ndiyo chuo cha mafunzo ya michezo, kitu ambacho sisi tunaweza tukasema mfumo huu sio mzuri umekuwa kama vile mabonanza na sio mashindano, kwa sababu huwezi kumuandaa mtoto shuleni kwa siku tano au kumi akawa imara katika michezo”, walisema.

Gideon Albert ambaye ni mmoja kati ya walimu walioshiriki mafunzo hayo kutoka Wilaya ya Mbinga Mkoani hapa alipohojiwa na waandishi wa habari alisisitiza kuwa ni lazima sasa tunapaswa kuwa na falsafa tofauti ya uchezaji mpira wa pete, huku akieleza kuwa wenzetu katika nchi ya Uganda wanaamini kwamba Fast Possesion ndiyo mbinu pekee ya kuweza kuboresha na kupata ushindi.

Albert aliongeza kuwa sisi Watanzania bado hatujawa na falsafa yoyote ya kukuza vipaji vya mchezo wa mpira huo na kwamba kila mmoja amekuwa na mifumo yake ambayo mwisho wa siku imekuwa ikiturudisha nyuma na kutufanya tushindwe kusonga mbele.

Naye Regina Ngahi ambaye ni mwalimu wa kutoka katika Manispaa ya Songea Mkoani humo alieleza kuwa mafunzo hayo ya makocha na waamuzi wa mpira huo wa Pete, wamefurahi kupata ujuzi wa mabadiliko ya sheria mpya zilizowekwa katika mchezo huo ambapo awali kutokana na kutoelewa walikuwa wakilazimika kutumia sheria za zamani ambazo zilikuwa zikiwarudisha nyuma kimchezo.

“Tumepata haya mafunzo inabidi sasa tukayatendee kazi kwa wanafunzi wetu wa Shule za msingi na sekondari na hata timu za mitaani katika maeneo ya kata zetu tunazoishi ili kuweza kuinua viwango vya michezo hapa nchini”, alisema Ngahi.

Aliongeza kuwa baada ya mafunzo hayo wanapata cheti ambacho kinawathibitisha kwamba wao watakuwa wakufunzi, waamuzi au makocha watakaoweza kuongoza timu ili hapo baadaye waweze kuunda timu moja.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Pete Tanzania (CHANETA) Mkoani Ruvuma, Janeth Duga alisema kuwa hapo awali sheria za mpira huo zilikuwa 21 lakini hivi sasa zipo 15 tu na kwamba wameandaa mafunzo hayo kwa ajili ya walimu hao ili kuweza kuwapatia ujuzi watakaoweza kwenda kuutumia kabla ya mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA hayajaanza ili waweze kupata na kutimia  sheria hizo mpya.

Janeth alisema kuwa baada ya kumaliza mafunzo walimu watarudi mashuleni na kwenda kuendesha mashindano hayo na kuandaa timu husika ambazo zitakutana makao makuu ya Mkoa huo kwa lengo la kutafuta timu ya Mkoa ambayo itawakilisha umoja huo wa michezo kwa shule za msingi na sekondari Mkoani humo.

“Mashindano haya rasmi yataanza mwezi wa tano mwaka huu yataendeshwa kwa muda wa wiki moja pale chuo cha ualimu Matogoro Songea na baadaye wale washindi watachaguliwa kwenda Mwanza kuwakilisha wenzao kwenye haya mashindano”, alisema Janeth. 

Hata hivyo mafunzo hayo yameshirikisha baadhi ya walimu wa kutoka Shule za msingi na sekondari katika Wilaya ya Mbinga, Nyasa, Tunduru, Namtumbo, Madaba, Mbinga mji na Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma ambapo walimu wengi walikuwa hawajui kwamba sheria za mpira huu wa pete zimebadilika kutokana na kuwa na mazoea ya kutumia sheria za zamani.

No comments: