Sunday, April 29, 2018

WAJASIRIAMALI WADOGO SONGEA WAPIGWA MSASA


Na Mwandishi wetu,      
Songea.

WAJASIRIAMALI wadogo 380 kutoka vikundi 67 vilivyopo Halmashauri ya Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma, wamepata mafunzo juu ya mbinu za uwekezaji katika viwanda vidogo.

Mafunzo hayo ambayo yamefanyika kwenye ukumbi wa Songea Klabu uliopo mjini hapa, yaliratibiwa na idara ya Maendeleo ya Jamii katika Manispaa hiyo na kufundishwa na watalaam mbalimbali wa taasisi na asasi za kifedha.

Akisoma taarifa ya vikundi hivyo Mkuu wa idara hiyo, Naftari Saioloyi alisema kuwa Manispaa ya Songea imekuwa na utaratibu wa kukopesha vikundi vya wanawake na vijana kutoka katika mapato yake ya ndani.


Saioloyi alieleza kwamba katika kipindi cha mwaka wa fedha wa 2017/2018 jumla ya vikundi 102 vilikopeshwa Shilingi milioni 116 kati ya hizo, vikundi 87 vya wanawake vilikopeshwa zaidi ya Shilingi milioni 101 na vikundi vya vijana 15 vilikopeshwa Shilingi milioni 14.9.

“Mikopo hii ililenga katika kila kikundi kuendeleza miradi ambayo ilianzishwa, leo hii Manispaa imeona ni vyema viongozi wa wanavikundi kukutana na wataalam kutoka taasisi za Serikali za SIDO, VETA, TICCIA ili wapate mafunzo na kuweza kupanua wigo wao wa uwekezaji’’, alisema Saioloyi.

Aliongeza kuwa mafunzo hayo yanalenga kuviwezesha vikundi hivyo kutafakari namna ya kufanya shughuli zao kulingana na maeneo wanayotoka, rasilimali walizonazo na upatikanaji wa soko kwa mazao watakayozalisha.

Akizungumza kabla ya kufungua mafunzo hayo Mkuu wa Wilaya ya Songea, Pololet Mgema alisisitiza kuwa mafunzo hayo ni muhimu hasa katika kutekeleza kauli mbiu ya Serikali inayolenga Tanzania ya viwanda kwa kila mkoa kuwa na viwanda 100.

Mgema alisema wajasirimali wadogo watakapofanikisha kwenye uwekezaji hata kama ni wa kiwanda kidogo watakuwa wamefikia kwenye malengo ya Taifa ya viwanda.

“Hakuna aliyezaliwa akaanza kutembea bali huanzia na kutambaa, kusimama halafu kutembea, kiwanda kidogo kinaanza na mtaji mdogo anzeni sasa ili baadaye mfikie hatua ya kufanya mabadiliko”, alisema Mgema.

Mafunzo hayo ya mbinu za uwekezaji katika viwanda vidogo yametolewa pia na taasisi za kifedha kutoka benki ya NMB, CRDB na POSTA.

No comments: