Sunday, April 29, 2018

SONGEA YAFANIKIWA KUPIGA CHAPA NG'OMBE 12,000


Na Kassian Nyandindi,     
Songea.

HALMASHAURI ya Wilaya ya Songea Mkoani Ruvuma imefanikiwa kupiga chapa ng’ombe zaidi ya 12,000 sawa na asilimia 69.6 waliostahili kupigwa chapa hadi kufikia Januari 31 mwaka huu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Simon Bulenganija aliwaeleza Waandishi wa habari kuwa utekelezaji huo umefanywa, kufuatia agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli la kutaka wapigwe chapa ili kuondoa tabia ya wafugaji kuingiza mifugo bila kufuata taratibu na sheria zilizowekwa.

“Kati ya ng’ombe 23,000 hapa Songea miongoni mwao ni ng’ombe 12,000 sawa na asilimia 69.6 ndio waliopitiwa na zoezi la upigaji chapa nawaomba wafugaji waendelee kujitokeza kwa wingi kutekeleza zoezi hili”, alisema Bulenganija.


Alibainisha kuwa Halmashauri hiyo bado inaendelea na zoezi hilo katika vijiji vyote 56 vilivyopo Wilayani humo na kwamba amewataka wafugaji kujitokeza kuwaleta ng’ombe wao ili waweze kupigwa chapa.

Kwa upande wake Afisa mifugo na uvuvi wa Wilaya hiyo, Ambangile Mwakabuka alisema kuwa changamoto inayowakabili hivi sasa ni uendeshaji wa zoezi hilo kutokana na wafugaji kuwa na uelewa mdogo, pamoja na uwepo wa baadhi ya miundombinu mibovu hali ambayo husababisha kushindwa kufikia lengo la asilimia mia moja katika utekelezaji wake hasa nyakati za masika.

Halmashauri ya Wilaya ya Songea ilizindua zoezi la upigaji chapa ng’ombe mnamo Agosti 10 mwaka jana katika kijiji cha Mhepai kata ya Kilagano na kutenga maeneo yaliyopimwa katika kijiji cha Magwamila hekta 8,000 na Mhepai hekta 20,000 kwa ajili ya malisho ya mifugo.

No comments: