Wednesday, April 4, 2018

NAMTUMBO YAPOKEA MILIONI 400 UJENZI MAJENGO KITUO CHA AFYA


Na Yeremias Ngerangera,    
Namtumbo.

HALMASHAURI Wilaya ya Namtumbo Mkoani Ruvuma, imepokea fedha Shilingi milioni 400 kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kwa ajili ya kuongeza, ujenzi wa majengo manne ya Kituo cha afya Namtumbo kilichopo Wilayani humo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisa habari wa Halmashauri hiyo inaeleza kuwa walipokea fedha hizo, mwezi Novemba mwaka jana na kwamba baada ya kutolewa taratibu za miongozo husika juu ya matumizi hayo utekelezaji unafanyika ili kuweza kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Baada ya kupitia miongozo ya matumizi ya fedha hizo Halmashauri imeanza ujenzi wa majengo hayo, katika Kituo cha afya Namtumbo kilichopo katika kata ya Rwinga mjini hapa.


Kwa mujibu wa maelezo ya Mhandisi wa majengo anayesimamia ujenzi huo Wilayani Namtumbo, Hassan Kinono alifafanua kuwa majengo yanayojengwa ni jengo la upasuaji, wodi ya akina mama wajawazito, maabara na nyumba ya kuishi mganga.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Christopher Kilungu aliongeza kuwa kutakuwa na ukarabati wa jengo la kuhifadhia maiti pamoja na ujenzi wa kichomea taka.

Ujenzi huo kwa ujumla wamekuwa wakitumia akaunti uwepo wa salio kwa kutumia akaunti ya nguvu ya jamii (Force account) na kupunguza matumizi makubwa ya fedha hizo ili kuweza kukarabati jengo hilo la maiti na kichomea taka katika kituo hicho.

Pamoja na mambo mengine Kituo cha afya Namtumbo kina wodi ya watoto, wodi ya wagonjwa, jengo la upasuaji akinamama wajawazito na jengo la kuhudumia wagonjwa wa nje ambapo hivi sasa ujenzi huo utasaidia kuboresha huduma za jamii.

No comments: