Friday, April 20, 2018

MACHINJIO HALMASHAURI MJI WA MBINGA YALALAMIKIWA KUKOSA MAJI YAKITHIRI KWA UCHAFU

Machinjio ya Halmashauri ya Mji wa Mbinga Mkoani Ruvuma, ambayo inalalamikiwa kukosa huduma ya maji na kushamiri kwa uchafu.

Na Kassian Nyandindi,     
Mbinga.

WACHINJAJI wa ng’ombe katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga Mkoani Ruvuma, wamesema kwamba wanashindwa kufanya kazi ya uchinjaji ng’ombe katika machinjio ya Halmashauri hiyo, iliyopo mjini hapa kutokana na kukosa huduma ya maji.

Aidha kufuatia uwepo wa tatizo la ukosefu wa huduma hiyo muhimu machinjio hiyo imekuwa katika hali mbaya kutokana na kukithiri kwa uchafu.

Wauzaji wa nyama ya ng’ombe mjini hapa nao jana wametia mgomo wa muda usiojulikana wakikataa kutoa huduma ya uchinjaji na uuzaji nyama, mpaka Mamlaka husika itakapoweza kutatua tatizo hilo ambalo limedumu kwa muda mrefu na kuwa kero kubwa.


Simon Mbunda ambaye ni mhudumu wa kufanya usafi katika machinjio hiyo aliwaeleza Waandishi wa habari kuwa, amekuwa akishindwa wakati mwingine kufanya usafi katika eneo hilo kutokana na kukosa vitendea kazi husika kama vile buti za kuvaa miguuni mwake.

Naye Mkaguzi wa nyama katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga, Geofrey Noel alisema kuwa wamezuia uchinjaji huo kuanzia Aprili 19 mwaka huu mpaka waweze kuwa na uhakika wa kupata huduma hiyo ya maji.

Alieleza kuwa tatizo kubwa la ukosefu wa maji kwenye machinjio hiyo linatokana na mfumo uliojengwa na Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Mji wa Mbinga (MBIUWASA) kutoleta maji ipasavyo katika matenki yaliyojengwa katika eneo hilo.

Noel alibainisha kuwa hata mafundi wa Mamlaka hiyo ya maji licha ya kupewa taarifa miezi kadhaa iliyopita juu ya hali hiyo, lakini wamekuwa wazembe kufanya ufuatiliaji na matengenezo madogo katika mfumo huo.

“Mafundi hawa wamekuwa hawafiki hapa mara kwa mara kufanya matengenezo madogo madogo pale tatizo linapojitokeza, wanakuja wanapotaka wao na tatizo la ukosefu wa maji katika machinjio hii lina muda mrefu sasa hakuna utekelezaji unaofanyika”, alisema Noel.

Naye Mwenyekiti wa Wachinjaji ng’ombe katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga, Joseph Chawala alisema kuwa licha ya kupeleka malalamiko yao mara kwa mara kwa uongozi wa Halmashauri ya Mji huo akishirikiana na Daktari wa mifugo wa Mji, hakuna utekelezaji uliofanyika kwa muda mrefu sasa.

Chawala alisema kuwa kwa siku za nyuma wamekuwa wakilazimika kuomba maji ya kisima nyumba jirani iliyopo karibu na machinjio hayo, jambo ambalo wamefikia hatua ya kuchoka na kuitaka Halmashauri itatue haraka tatizo hilo, kwani wamekuwa wakikusanya ushuru kupitia uchinjaji pale unapofanyika.   

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Mbinga, Robert Mageni alipotafutwa ili aweze kutolea ufafanuzi juu ya changamoto hizo hakuweza kupatikana Ofisini kwake.

No comments: