Waziri wa nishati na madini, Profesa Sospeter Muhongo. |
Na Mwandishi wetu,
Kagera.
BAADHI ya Wateja ambao wamelipia huduma ya kuunganishiwa nishati
ya umeme majumbani kwao wilaya ya Biharamulo mkoa wa Kagera, wamelinyoshea
kidole Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) wilayani humo kwa kushindwa
kutimiza majukumu yake kwa wakati na kuwafanya wateja hao, wapate hasara katika
kuendesha shughuli zao za ujasiriamali.
Aidha imeelezwa kuwa wateja hao ambao ni wa maeneo ya mjini wamelilalamikia
Shirika hilo wakidai kwamba, tokea walipolipia huduma ya kujengewa mita za
umeme mwanzoni mwa mwezi wa sita mwaka huu, hakuna utekelezaji uliofanyika
jambo ambalo linawafanya wawe na mashaka.
Wakizungumza na mwandishi wetu kwa nyakati tofauti, walisema
kuwa shughuli zao za ujasiriamali ambazo zinategemea nishati hiyo ya umeme
wanashindwa kuziendesha, hivyo wanaiomba serikali itatue kero hiyo mapema ili
waweze kuondokana na adha kubwa wanayoipata sasa.
Kadhalika wamemuomba Waziri mwenye dhamana, Profesa Sospeter
Muhongo kuona umuhimu wa kuingilia kati ili kuweza kumaliza tatizo hilo mapema ambalo
hawajui litakwisha lini.