Na Yeremias Ngerangera,
Namtumbo.
PAMOJA na Serikali kuendelea kusisitiza wahalifu wanaowapatia
mimba wanafunzi wa kike kufungwa miaka thelathini jela, bado baadhi ya jamii imekuwa ikiendelea na
tabia hiyo kitendo ambacho kimekuwa kikikatisha ndoto za maendeleo ya maisha
kwa watoto hao.
Aidha wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma, tabia hiyo imekuwa
ikiendelea kufanyika licha ya viongozi husika wilayani humo kukemea kwa nguvu
na kupiga marufuku baada ya kuona kwamba imekuwa ikitishia maendeleo ya
wanafunzi hao.
Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wetu umebaini kuwa tatizo
hilo limekuwa likiendelea kushamiri wilayani hapa, kutokana na jamii kutotoa
ushirikiano wa kutosha kwa serikali hasa pale inapotaka kusimamia sheria ikiwemo
kuwafikisha Mahakamani watuhumiwa wenye tabia hiyo.
Imeelezwa kuwa baadhi yao wamekuwa wakishindwa kutoa ushirikiano
wa kutosha badala yake ndiyo wamekuwa chanzo cha kuvuruga madai husika yasiweze
kusonga mbele katika vyombo vya sheria ikiwa ni lengo la kuepuka kufungwa miaka
30 jela.