Friday, May 10, 2013

MADEREVA WA DALADALA KATIKA MJI WA IRINGA WAGOMA KUSAFIRISHA ABIRIA, POLISI WAINGILIA KATI KUWATULIZA

Baadhi ya abiria wakiwa wamepanda gari ya mizigo mjini Iringa, kwa lengo la kuwahi katika maeneo yao ya kazi leo, baada ya madereva wa daladala kugoma kusafirisha abiria.

Na Mwandishi wetu,
Iringa.

KWA siku ya leo kadhia za hapa na pale zimeanza kujitokeza katika mji wa Iringa, mkoani Iringa kufuatia mgomo wa daladala ambao umeanza kwa kasi na kuchukua sura mpya, hali ambayo imesababisha wananchi, kutembea kwa mguu umbali mrefu wakielekea katika maeneo yao ya kufanyia kazi.

Mgomo  wa  daladala  umeanza  kwa  kasi katika mji  wa Iringa baada ya daladala  zote  kugoma  kufanya kazi, huku wanafunzi na wafanyakazi wa iadara mbalimbali wakichelewa kwenda katika vituo vyao vya kazi.

   
Hali  hiyo ya mgomo  imeanza  kutikisa  na kufanya  polisi  kuingilia kati  kuwatuliza  madereva  wasigome jitihada ambazo zinaendelea  hadi  sasa.

Mwandishi wetu ambaye yupo katika maeneo mbalimbali ya mji huu, ameshuhudia hali jinsi ilivyo ambapo watu wanalazimika kupanda hata magari ya kubebea mizigo, ili waweze kufika katika vituo vyao vya kazi.

Machungu ya mgomo huu kwa kiasi kikubwa yameathiri maeneo mbalimbali ya mji wa Iringa, ambapo usafiri ambao umeonekana ukifanya kazi sasa ya kusafirisha abiria ni bajaji, pikipiki na taxi huku nauli kwa mtu mmoja katika bajaji  shilingi 3000 wakati taxi kwa kila kichwa shilingi 1000 hali ambayo wananchi wengi wenye kipato cha chini wanaonekana kushindwa kumudu gharama hizo.

Hadi habari hizi zinaenda mitamboni chanzo cha mgomo huo kinatokana na madereva wa daladala katika mji huo kuzuiwa kuchukua abiria katika kituo kimoja kilichopo mjini hapa, badala yake wanaruhusiwa kushusha abiria tu na sio vinginevyo.

Vilevile baadhi ya abiria walikuwa wakiwalalamikia madereva hao  kwamba, wamekuwa wakitoza fedha mara mbili endapo anatoka kituo kimoja kwenda kingine, jambo ambalo limesababisha adha hiyo kujitokeza.

No comments: