Tuesday, May 14, 2013

VIGOGO WILAYANI MBINGA WASHUSHIWA SHUTUMA NZITO, MKUU WA WILAYA ANYOSHEWA KIDOLE, MKURUGENZI MTENDAJI ADAIWA KUWA KINARA WA KUENDELEZA MGOGORO

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu.





















Na Kassian Nyandindi,

Mbinga.


KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida baadhi ya viongozi Waandamizi wa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma, wamenyoshewa kidole na kulalamikiwa kwamba, wamekuwa wakifumbia macho malumbano yanayoendelea kushamiri katika idara ya elimu wilayani humo.

Aidha vigogo hao wilayani humo, wametupiwa lawama kwamba wengine wamekuwa wakishiriki katika kuendeleza malumbano hayo, na hata kufikia hatua ya kukatisha tamaa kwa baadhi ya watendaji wa idara hiyo, ambao wanaonekana kufanya vizuri katika kukuza maendeleo ya sekta hiyo ya elimu.

Kwa ujumla hivi sasa kumekuwa na mgogoro mzito katika idara ya elimu wilayani Mbinga, hasa kwa kitengo cha elimu ya msingi jambo ambalo linazua malalamiko kutoka miongoni mwa wadau wa elimu.

Madai hayo yalitolewa leo kwenye kikao cha tathimini ya Wadau wa elimu, kilichoketi kwenye ukumbi wa Jimbo la Mbinga, Kanisa katoliki uliopo mjini hapa ambacho kilikuwa kikiongozwa na Mwenyekiti wake, ambaye ni Mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga.

Sambamba na hilo Mwenyekiti wa huduma za jamii wilayani Mbinga James Yaparama, alimnyoshea kidole Mkuu wa wilaya hiyo Senyi Ngaga akisema tatizo hili lipo katika ofisi yake na analifahamu, lakini inashangaza kuona mhusika anayeendeleza mgogoro huo kutochukuliwa hatua za kisheria.

“Mheshimiwa mkuu wa wilaya, kuna kigugumizi gani kilichopo ambacho mtu anayetuvuruga unamfahamu na unashindwa kuchukua hatua za kisheria dhidi yake?, tunaishia kuunda tume ya kuchunguza tatizo hili na kumaliza hela za halmashauri kwa kulipana posho juu ya jambo hili, wakati lipo wazi linajulikana”, alisema James Yaparama.

Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA) Desderius Haulle akichangia hoja katika kikao hicho, alimshushia shutuma nzito Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya Mbinga Shaibu Nnunduma kwa kile alichoeleza kuwa, ndiye kinara namba moja anayehusika katika kuendeleza mgogoro huo huku akijua kwamba hilo ni kosa kwa mujibu wa sheria za utumishi wa umma.

Desderius Haulle baada ya kutamka hilo alimtaka Mkuu wa wilaya hiyo kuchukua hatua mapema, kwa kulifanyia kazi huku akieleza kuwa habari zinazozungumzwa na wadau wa elimu katika maeneo mbalimbali wilayani Mbinga, kwamba Mkurugenzi huyo wa halmashauri ya wilaya hiyo kwa kiasi kikubwa amekuwa ndio chanzo cha mgogoro huo. 

"Mheshimiwa mkuu wa wilaya hiki ambacho kinafanywa na mkurugenzi huyu si cha kukifumbia macho, ni vyema hatua sasa zichukuliwe kwa kulifanyia kazi haraka", alisisitiza Desderius Haulle.

 Diwani wa viti maalum Tarafa ya Mbinga mjini Grace Millinga aliendelea kupigilia msumali wa moto akisema, katika kipindi cha miaka ya nyuma malumbano haya hayakuwepo lakini watu wachache tu ndio wanaonekana kutaka kurudisha nyuma sekta ya elimu wilayani humo, kwa maslahi yao binafsi.

“Leo hii malumbano haya yanafanywa na baadhi ya watumishi ambao si wazawa wa wilaya hii, sisi tuna uchungu sana, kwa niaba ya wenzangu tunasema hatutakubali kuvumilia hali hii iendelee tunapoona wenzetu hawa wanaturudisha nyuma”, alisema Grace Millinga.

Diwani huyo alieleza kuwa kundi hilo la watu wachache kazi yao ni kupiga majungu tu, huku akiongeza mbele ya mkuu huyo wa wilaya ya Mbinga kwamba, kama hali hiyo itaendelea kufumbiwa macho ipo siku yeye yupo tayari kulitaja jina la mtu anayehusika katika malumbano hayo ya kurudisha nyuma sekta ya elimu wilayani humo.

“Huyu mtu mheshimiwa mkuu wa wilaya ofisi yako inamfahamu, unao uwezo wa hata kumwajibisha kwa namna moja au nyingine ikiwemo hata kumhamisha akafanyie kazi maeneo mengine, kwa nini usituondolee huyu mtu?”, alihoji Grace Millinga.

Kadhalika Mratibu wa elimu kata ya Luwaita Laurent Nsuha alisema kumekuwa na barua zinazoendelea kuandikwa na kumchafua ofisa elimu shule za msingi ambazo hazina msingi wa aina yoyote ile, hali ambayo imekuwa ikikatisha tamaa na kurudisha nyuma maendeleo ya sekta ya elimu wilayani Mbinga.

“Mheshimiwa mkuu wa wilaya, ninyi viongozi waandamizi mnapaswa kutoa ushirikiano juu ya tatizo hili kwa kulifanyia kazi haraka, na sasa nashauri hebu tukae na kuangalia tunaendesha vipi mustakabali wa maendeleo ya elimu kwa shule zetu za msingi hapa wilayani, inakuwa si vyema viongozi wachache kulumbana kwa maslahi binafsi, lakini tunafahamu na ninyi viongozi waandamizi mpo katika mgogoro huu”, alisema Laurent Nsuha.

Naye Diwani wa kata ya Mbinga mjini Kelvin Mapunda alisema mahusiano kwenye ofisi za vigogo wa ngazi ya wilaya, sio mazuri hivyo wao kama wadau wa elimu wanaona wanakoipeleka jamii hii ya wanambinga sio kuzuri, kutokana na kuendeleza migogoro isiyokuwa ya lazima.

Kwa upande wake mkuu  wa wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga akijibu malalamiko hayo katika kikao hicho cha wadau wa elimu alisema, “Ni kweli barua za migogoro juu ya tatizo hili ofisi yangu na kamati yangu ya ulinzi na usalama tumeziona na tunaendelea kuzifanyia kazi”.

Senyi Ngaga alifafanua kuwa ofisi yake imekwisha anza pia kukaa vikao na maofisa husika kutoka idara ya elimu wilayani humo, hivyo anachohitaji zaidi ni ushirikiano wa kutosha kutoka kwa wadau mbalimbali, katika kumaliza mgogoro huo.

Wakizungumza na Mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti na sharti la kutotajwa majina yao katika mtandao huu, wadau hao wa elimu walisema kuwa mgogoro huo unasababishwa na baadhi ya viongozi wenye uchu wa madaraka na tamaa ya fedha ambazo ni malimbikizo ya walimu ya likizo na uhamisho kwa shule za msingi, ambao wamekuwa na tabia ya huko katika miaka ya nyuma wakizichota na kuzitumia kinyume na taratibu kwa maslahi yao binafsi.

Walifafanua kuwa kutokana na afisa elimu wa shule za msingi wilayani Mbinga, Daud Mathias Mkali kujenga msimamo wake wa  matumizi mazuri ya fedha hizo na kuhakikisha walimu wanalipwa stahiki zao ipasavyo na kwa wakati, ndio maana kunazua malumbano na kuandikiana barua za hapa na pale kwa lengo la kutaka kumchafua ili hatimaye serikali au uongozi husika ufanye taratibu za kuweza kumhamisha na kumpangia kituo kingine cha kufanyia kazi, ili wao waweze kupata mwanya wa kupanga safu ya kumweka madarakani ofisa elimu wanayemtaka wao na hatimaye wafanikiwe kuchota fedha hizo kama walivyozoea katika miaka hiyo ya nyuma.

Hata hivyo, miaka mitano iliyopita wilaya ya Mbinga kwa upande wa ufaulu wa elimu ya msingi hali ilikuwa tete na sasa baada ya serikali kufanya utaratibu wa kuleta ofisa elimu mwingine, mabadiliko katika sekta hii muhimu yamejitokeza na sasa wilaya ya Mbinga imekuwa ikishika nafasi ya tatu kimkoa tofauti na miaka kadhaa ya nyuma ilikuwa ikishika mkia.

No comments: