Monday, May 6, 2013

SHAMBULIO LA KIGAIDI LILILOTOKEA ARUSHA, RAIS AKATIZA ZIARA YAKE NCHINI KUWAIT

 


 


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete leo, Jumatatu, Mei 6, 2013, ameamua kukatiza ziara yake ya Kiserikali nchini Kuwait ili kurejea nyumbani kutokana na tukio la shambulio la kigaidi la mlipuko mjini Arusha ambako watu wawili wamefariki na 60 wamejeruhiwa.

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu ya Dar es Salaam, imesema Rais Kikwete aliyekuwa aondoke arejee nyumbani kesho, amelazimika kukatiza ziara hiyo na anaondoka Kuwait City kurejea nyumbani mara moja ili kuwa karibu na wafiwa pamoja na wale waliojeruhiwa katika shambulio hilo la kigaidi.

Miongoni mwa shughuli ambazo hazitafanyika sasa kutokana na uamuzi huo wa Rais ni ziara ya kutembelea Kampuni ya Mafuta ya Kuwait katika  eneo la Ahmadi mjini Kuwait. Aidha, Rais hatahudhuria dhifa ya chakula cha jioni ambacho alikuwa anaandaliwa na Waziri Mkuu wa Kuwait, Mheshimiwa Sheikh Jaber Al Mubarak Al Hamad Al Sabah.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
6 Mei, 2013

 

No comments: