Friday, May 3, 2013

MKUU WA MKOA WA ARUSHA ATISHIA WAANDISHI WA HABARI, ASEMA ATAKAYEIGUSA SERIKALI ATAKUWA AMEIWEKA ROHO YAKE REHANI

Mkuu wa mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo.


















Na Mwandishi wetu,

Arusha.

MKUU wa mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo ametoa onyo kali kwa waandishi wa habari nchini, kwamba yeyote atakayeishambulia na kuikosoa au kuigusa serikali atakiona cha mtema kuni.

Mulongo amesema yupo tayari kushirikiana na waandishi wa habari Tanzania, lakini atakaye thubutu kuigusa serikali atakuwa ameiweka roho yake rehani.

Mpaka sasa haijafahamika kwa nini RC huyo ametoa kauli hiyo, lakini wadadisi wa masuala ya siasa wanasema kwamba Mulungo amelazimika kutoa kauli hiyo kutokana na kutofautiana na Mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema ambaye sasa ameshitakiwa kwa uchochezi.


Awali baada ya kuuawa kwa mwanafunzi wa chuo cha uhasibu Arusha (IAA) na kutokea vurugu na kuzomewa kwa mkuu wa mkoa huo, aliamuru Lema kukamatwa na kufunguliwa kesi ya uchochezi.

Wataalamu wengine wa siasa wanasema kwamba Mulongo ametoa kauli hiyo kali
kwa madai kwamba, waandishi wa habari waliandika zaidi taarifa za Lema kuliko za mkuu wa mkoa huyo.

Akihutubia katika sherehe za siku ya Wafanyakazi alisema ikibainika kwamba waandishi wa habari wanatumika, nao wanatumika  watafikishwa katika vyombo vya sheria.

Mulongo alisema kwamba vitu vilivyoandikwa si kweli na kwamba wataendelea kufuatilia kwa kuwa baadhi ya waandishi mkoani humo, wamekuwa wakifanya kazi  zao kwa ushabiki wa kisiasa na kuandika mambo ambayo hawana uhakika nayo.

"Unapoingia katika mkakati wa kudhalilisha kiongozi wa serikali, unakuwa umeiweka roho yako rehani, kuweni makini," alisema Mulongo.

Hata hivyo wadau mbalimbali wa habari waliozungumza na mwandishi wa habari hizi walisema, kauli hiyo ya kitisho iliyotolewa na mkuu huyo wa mkoa dhidi ya waandishi wa habari, haifai katika jamii na kwamba hizi ni zama za uwazi na ukweli hivyo, yeye hana nguvu ya kuviziba vyombo vya habari katika kutekeleza majukumu yake.

No comments: