Wednesday, May 22, 2013

WAKAZI WA TINGINYA WILAYANI TUNDURU WANUFAIKA NA MFUMO WA UMEME JUA

Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Chande Nalicho.



Na Steven Augustino,

Tunduru.

WAKAZI wa kijiji cha Tinginya tarafa ya Nakapanya wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, wameipongeza serikali kwa kuwafungia mfumo wa umeme Jua(SOLA) katika zahanati yao na kueleza kuwa mradi huo, utawakomboa wanawake ambao kwa muda mrefu walikuwa wakijifungua wakiwa gizani.

Fatuma Mapila na Alihad Abdalahman ambao walikuwa wamepeleka mtoto wao kwa ajili ya matibabu na muuguzi wa zahanati hiyo, Grolia Lupindo ni miongoni mwa baadhi ya wananchi ambao walishindwa kuzuia furaha yao, baada ya kushuhudia wakati mfumo huo ukiwashwa katika zahanati yao na katika nyumba ya mganga, iliyopo jirani na eneo hilo la kutolea huduma ya afya.

Wakizungumza kufuatia hali hiyo walisema,  kwa muda mrefu tangu zahanati yao ifunguliwe mwaka 1990 na kuanza kutoa huduma, wanawake wa kijiji cha Tinginya na vitongoji jirani walikuwa wakitumia vijinga vya moto kumulikia wakati wa kujifungua, hali ambayo ilikuwa ikihatarisha maisha yao na watoto wanaojifungua.

Awali akizungumza na wananchi hao afisa mafunzo na ujengaji wa uwezo kutoka wakala wa nishati Vijijini(REA) Mary Ngusaru alisema, ufungaji huo wa mfumo wa umeme jua umefanywa na vijana 35 waliomaliza mafunzo ya siku 7 na kwamba hivi sasa wilaya ya Tunduru, imepata hazina ya mafundi wenye uwezo wa kufunga mfumo huo na kufanya matengenezo madogo mdogo wakati  kunapotokea hitilafu.

Ngusaru alifafanua kuwa hadi kukamilika kufungwa kwa mfumo huo na mfumo mwingine utakaofungwa katika zahanati ya kijiji cha Nampungu,  utagharimu jumla ya shilingi milioni 20 ambazo zimetolewa na serikali kupitia mpango wa changamoto za milenia (MCC).

Naye mwezeshaji wa mafunzo hayo  mhandisi  Philbert Beyanga kutoka kampuni ya Solar Energy alisema, katika kipindi hicho vijana hao  wamenolewa na kupatiwa ujuzi huo ikiwemo uendelezaji wa teknolojia ya umeme jua, nishati upepo, na nishati ya maporomoko ya maji.

Alisema mfumo wa umeme jua katika zahanati ya kijiji hicho ambao umejengwa, unao uwezo wa kuwasha taa 36 pamoja  kumudu kuendesha mashine za kupimia ugonjwa wa Malaria, jambo ambalo litarahisisha utendaji wa kazi kwa watumishi wa zahanati hiyo.


No comments: