Thursday, May 2, 2013

MGODI WA MAKAA YA MAWE NGAKA, WAFUNGWA WANANCHI WAMTAKA MBUNGE WA MBINGA MASHARIKI AJIUZURU

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete.
Matrekta yakifanya kazi ya kuchimba mkaa wa mawe katika mgodi wa Ngaka uliopo kijiji cha Ntunduaro kata ya Ruanda wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma.


Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

MKUU wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu,  amelazimika kuufunga kwa muda usiojulikana, mgodi wa makaa ya mawe Ngaka uliopo katika kijiji cha Ntunduaro kata ya Ruanda wilayani Mbinga mkoani humo, baada ya wananchi wa kijiji hicho kumtaka mkuu huyo wa mkoa aufunge mgodi huo mpaka watakapolipwa madai yao ya muda mrefu ya fidia wanazodai, pamoja na kuyaweka mazingira yao katika hali inayostahili kwa matumizi ya binadamu.

Mradi huo wa makaa ya mawe unamilikiwa na kampuni ya ubia ya Tancoal Energy, ambayo asilimia 30 ya hisa zake zinamilikiwa na serikali kupitia shirika la maendeleo la Taifa NDC, na asilimia 70 ya hisa zinamilikiwa na mwekezaji wa kampuni ya Intra Energy.

Mwambungu alichukua uamuzi huo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa shule ya msingi Ntunduaro, ambao ulihudhuriwa na umati mkubwa wa wananchi wa kijiji hicho, wakiwemo viongozi wa kamati ya ulinzi na usalama ngazi ya wilaya ya Mbinga  na Mkoa wa Ruvuma, pamoja na viongozi wa vyama vya siasa.



Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Senyi Ngaga alimkaribisha mkuu wa mkoa huo Mwambungu, ili azungumze na wananchi kuhusu mgogoro uliopo kati ya wananchi na mwekezaji wa mgodi huo.

Baada ya kukaribishwa mkuu huyo wa mkoa alianza kwa kusema “wananchi wa Ntunduaro hoyee! wananchi wakajibu hoiiii! huku wakipaza sauti zao, mpaka kieleweke”.

Kwa ujumla hali ilikuwa tete ambapo  Mwambungu  aliwataka wananchi hao kuwa watulivu, wakati anapotaka kuwaambia nini serikali yao imefanya katika kumaliza tatizo hilo.

Pamoja na mkuu huyo wa mkoa kujaribu kuwatuliza wananchi hao, bado hali iliendelea kuwa mbaya baada ya wananchi kumshinikiza Mwambungu  waende nae mpaka kwenye eneo la mgodi akaufunge na kama haitawezekana basi wapo tayari kufa kwa kupigwa risasi kuliko kufa kwa njaa wakati haki zao zipo na zinadhulumiwa na watu wachache.

Wananchi hao walisema matatizo na dhuluma iliyopo yanasababishwa na viongozi wa serikali huku baadhi yao wakiugua magonjwa mbalimbali kutokana na  kunywa maji yenye chembechembe ya sumu ya madini ya makaa ya mawe yanayochimbwa eneo la kijiji hicho.

Mto Nyamabeva uliopo katika kijiji hicho ambao ndio tegemeo kubwa, maji yake yamechafuliwa na wawekezaji hao kutokana na mkaa wa mawe.

Akitoa kero mbele ya mkuu wa mkoa mwananchi Erick Mapunda alisema kuwa wamechoka na ahadi hewa za mwekezaji wa mgodi huo, ambazo kila kukicha imekuwa ni siasa hivyo ujio wa mkuu huyo wa mkoa uwe ni hitimisho la kwenda kuufunga mgodi, mpaka hapo watakapotimiziwa ahadi walizoahidiwa pamoja na kuwalipa fidia wanazoidai kampuni ya Tancoal Energy.


Naye Joseph Messa alieleza kuwa yeye akiwa ni mwananchi wa kijiji hicho, amekata tamaa ya maisha kwa sababu hali ya kijiji chao ni mbaya kwa sasa, kutokana na kukosekana kwa miundo mbinu ya barabara, maji, shule pamoja na zahanati kwani watoto wao wamekumbwa na magonjwa ya kichocho ambayo hawajui yanasababishwa na nini na kwamba wamekuwa wakinywa maji ya sumu tangu mgodi huo uanze kufanya kazi, licha ya kuwa malalamiko hayo walikwisha yafikisha kwa viongozi wa serikali ya kijiji, wilaya na mkoa.

Alisema inasikitisha kuona viongozi hasa ngazi ya wilaya walikuwa wakionekana mara kwa mara kutembelea eneo la mgodi, na alidai kuwa yawezekana wamejenga urafiki mkubwa na mwekezaji wa mgodi huo na ndio maana kero zao zilikuwa hazifanyiwi kazi.

Kwa upande wake  Benedina Komba alisema kuwa tangu mgodi huo uanze kufanya kazi wananchi wa kitongoji cha Nkaya, walipewa ahadi ya kuhama maeneo yao kwa muda kwa madai kuwa wataonyeshwa maeneo mengine ambayo wangepewa fidia ili wakajenge nyumba za kuishi,  jambo ambalo mpaka sasa halijatekelezwa na hivi sasa wamebaki wakihangaika na watoto wao kutokana na njaa kwa kuwa eneo walilokuwa wakilima mazao mbalimbali limechukuliwa na kampuni hiyo inayochimba makaa ya mawe.

Wosteri Mapunda alielekeza shutuma nzito kwa waandishi wa habari wa mkoa wa Ruvuma kwa kutoandika habari za mgogoro huo, tofauti na waandishi wa mkoa wa Arusha ambao wamekuwa wakiandika habari za mgogoro wa Loliondo, ambapo serikali baada ya kusikia kwenye vyombo vya habari ilihamia huko, ili kumaliza mgogoro uliopo na kwa nini Ntunduaro ishindikane kwa muda wa miaka mitatu sasa.


Aidha  Johoni Nyimbo alimnyooshea kidole Mbunge wa jimbo la mbinga mashariki  Gaudence Kayombo na kumkumbusha ahadi aliyowaahidi wananchi wa kijiji hicho, Mei 19 mwaka 2011 kwenye mkutano wa hadhara kuwa endapo wanakijiji hao hawatalipwa fidia wanazodai atajiuzuru nafasi aliyonayo ya Ubunge, na kumtaka ajiuzuru nafasi hiyo mara moja jambo ambalo lilimpandisha hasira na  baada ya kauli iyo alilazimika kusimama ili kutoa ufafanuzi wa kauli yake hali ambayo ilisababisha kuwapandisha hasira wananchi hao na kuanza kumzomea.

Hata hivyo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) mkoa wa Ruvuma, Oddo Mwisho naye alikumbwa na adha ya kuzomewa baada ya  kusimama na kuanza kujieleza kuhusiana na jitihada za chama cha mapinduzi na serikali yake ya wilaya na mkoa huo, kwamba kwa muda mrefu wamekuwa wakifanya mazungumzo kupitia Wizara ya nishati na madini, Shirika la maendeleo la Taifa(NDC) pamoja na mwekezaji wa kampuni ya Tancoal Energy, kwa lengo la kumaliza mgogoro uliopo kati ya mwekezaji na wananchi.


Kufuatia vurugu zilizojitokeza kwenye mkutano huo mkuu wa mkoa  Mwambungu alilazimika kusitisha mkutano huo kwa muda na kuwataka wananchi hao warudi eneo la mkutano baada ya nusu saa, ili apate nafasi ya kujadiliana na kamati yake ya ulinzi na usalama na baadae baada ya nusu saa kupita, mkutano ulianza ambapo mkuu huyo wa mkoa wa Ruvuma, aliwaeleza wananchi hao kuwa amesikia maoni yao na amefikia hatua ya kuufunga mgodi huo kwa muda usiojulikana hadi hapo madai yao ya msingi yatakapofanyiwa kazi na kutekelezwa.

Kwa ujumla mgogoro uliopo kati ya mwekezaji wa mgodi huo na wananchi wa kijiji cha Ntunduaro unatokana na kampuni ya Tancoal Energy kutokamilisha kwa muda mrefu kazi waliyoahidi ya ukarabati wa zahanati ya kijiji hicho, ujenzi wa visima vya maji, shule na ulipaji wa fidia kwa wananchi 306 ambao wamefanyiwa tathimini.

Pia madai mengine ni kwamba zaidi ya wananchi 400 ambao awali walilipwa fidia zao, ilionekana fedha walizolipwa ni kidogo hivyo nao walipewa ahadi ya kuongezewa malipo mengine, jambo ambalo hadi leo hii halijatekelezwa.






















No comments: