Monday, May 6, 2013

MWEKEZAJI MGODI WA MAKAA YA MAWE MBINGA ARUHUSIWA KUENDELEA NA KAZI, MKUU WA MKOA AKIRI WANANCHI KUNYWA MAJI YENYE SUMU

Mtambo maalum, ukifanya kazi ya kuchimba makaa ya mawe huko kijiji cha Ntunduaro kata ya Ruanda wilayani Mbinga, mkoa wa Ruvuma.


Na Kassian Nyandindi

Mbinga.

MGODI wa makaa ya mawe Ngaka uliopo katika kijiji cha Ntunduaro kata ya Ruanda, wilayani Mbinga mkoa wa Ruvuma ambao ulifungwa kwa muda usiojulikana sasa umefunguliwa rasmi, na mwekezaji husika ameruhusiwa kuendelea na shughuli za uchimbaji wa makaa hayo.

Ufunguzi huo umefanyika hivi karibuni Mei 3 mwaka huu majira ya mchana na mkuu wa mkoa wa Ruvuma Said Mwambungu, ambaye ndiye aliyeufunga Aprili 30 mwaka huu.

Mwambungu alitoa kauli ya kuufungua mgodi huo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa eneo la ofisi za kijiji cha Ntunduaro, ambao ulihudhuriwa na umati mkubwa wa wananchi wa kijiji hicho, wakiwemo viongozi wa kamati ya ulinzi na usalama ngazi ya wilaya ya Mbinga  na mkoa wa Ruvuma, pamoja na viongozi wa vyama vya siasa.


Akihutubia katika mkutano huo, mkuu huyo wa mkoa alisema uamuzi wa kufungua mgodi wa makaa ya mawe Ngaka umetokana na makubaliano yaliyofanyika na mwekezaji wa mgodi huo, kwamba katika kipindi cha siku 45 kuanzia Mei 4 mwaka huu, mwekezaji husika anatakiwa kukamilisha kazi ya ujenzi wa miundombinu ya maji safi na salama na kuisambaza katika makazi ya wananchi wa kijiji hicho.

Aidha juu ya madai ya fidia ya wananchi hao, mwekezaji pia amepewa siku 45 kuhakikisha kila mtu anayedai awe amelipwa na mwisho wa malipo ni June 15 mwaka huu.

Licha ya mkuu huyo wa mkoa kutoa tamko hilo la kuufungua mgodi, baadhi ya kundi la wananchi lilionekana kupinga wakidai usifunguliwe hadi madai yao ya msingi yatakapotekelezwa, lakini Mwambungu na kamati yake ya ulinzi na usalama aliyoongozana nayo waliendelea kuwasihi wananchi hao na ndipo walipofikia uamuzi wa makubaliano kwamba ufunguliwe.

Akizungumza na waandishi wa habari Mwambungu alikiri pia wananchi wa kijiji hicho kunywa maji yenye sumu ya chembechembe za mkaa wa mawe, huku akiongeza kuwa wana haki ya kulalamika juu ya tatizo hilo.  

Awali kufungwa kwa mgodi huo wa makaa ya mawe kulitokana na wananchi wa kijiji cha Ntunduaro, kumtaka mkuu huyo wa mkoa aufunge mpaka watakapolipwa madai yao ya muda mrefu ya fidia wanazodai, pamoja na kuyaweka mazingira yao katika hali inayostahili kwa matumizi ya binadamu.

Mradi huo wa makaa ya mawe unamilikiwa na kampuni ya ubia ya Tancoal Energy, ambayo asilimia 30 ya hisa zake zinamilikiwa na serikali kupitia shirika la maendeleo la Taifa NDC, na asilimia 70 ya hisa zinamilikiwa na mwekezaji wa kampuni ya Intra Energy.

Kwa ujumla siku ambayo mkuu huyo wa mkoa alichukua uamuzi wa kuufunga mgodi huo, hali ilikuwa tete ambapo wananchi walikuwa wakipiga kelele na kutoa vitisho wapo tayari hata kufa kwa kupigwa risasi endapo madai yao ya msingi hayatatekelezwa, na haki zao zipo na zinadhulumiwa na watu wachache.

Wananchi hao walikuwa wakipaza sauti zao wakisema matatizo na dhuluma iliyopo yanasababishwa na viongozi wa serikali, huku baadhi ya wananchi wakiteseka na kuugua magonjwa mbalimbali kutokana na  kunywa maji yenye chembechembe ya sumu ya madini ya makaa ya mawe, yanayochimbwa katika eneo la kijiji hicho.

Mto Nyamabeva uliopo katika kijiji hicho ambao ndio tegemeo kubwa, maji yake yamechafuliwa na wawekezaji hao kutokana na vumbi la mkaa wa mawe.

Kwa ujumla mgogoro uliopo kati ya mwekezaji wa mgodi huo na wananchi wa kijiji cha Ntunduaro unatokana pia na kampuni hiyo ya Tancoal Energy kutokamilisha kwa muda mrefu kazi waliyoahidi ya ukarabati wa zahanati ya kijiji hicho, ujenzi wa visima vya maji, shule na ulipaji wa fidia kwa wananchi 306 ambao wamefanyiwa tathimini.

Hata hivyo madai mengine ni kwamba zaidi ya wananchi 400 ambao awali walilipwa fidia zao, ilionekana fedha walizolipwa ni kidogo hivyo nao walipewa ahadi ya kuongezewa malipo mengine, jambo ambalo hadi leo hii halijatekelezwa.

No comments: