Thursday, May 23, 2013

VURUGU ZA MTWARA: VIKAO VYA BUNGE VYA ENDELEA KUAHIRISHWA, NYUMBA YA MWANDISHI WA HABARI YACHOMWA MOTO

Spika Anna Makinda akizungumza na Wabunge Dodoma leo.
























BUNGENI DODOMA:

HALI imekuwa tete mkoani Mtwara kufuatia mapambano ya wananchi na askari wa Jeshi la Polisi yakiendelea mkoani humo, ambapo Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda amelazimika kuahirisha vikao vya Bunge kwa siku ya pili sasa, ili kuipa serikali nafasi ya kumaliza mgogoro huo ambao unaendelea.

Spika huyo alifikia maamuzi hayo leo asubuhi baada ya Waziri wa mambo ya ndani ya nchi Dkt. Emmanuel Nchimbi, kutoa maelezo ya serikali juu ya mapigano hayo yaliyoanza jana mkoani humo.

Wananchi wa Mtwara walianzisha mapigano hayo kwa lengo la kupinga hotuba ya Wizara ya nishati na madini, iliyosomwa Bungeni na kuweka msisitizo kwamba gesi hiyo lazima isafirishwe hadi Jijini Dar es Salaam.


Akiahirisha vikao hivyo vya Bunge la bajeti Makinda alisema, endapo ataruhusu wabunge wajadili maelezo ya serikali yaliyotolewa na Waziri Dkt. Nchimbi, hali hiyo itazidi kuchochea mapigano hayo.

"Baada ya kusikiliza maelezo ya serikali, naomba kuahirisha vikao vya bunge hadi kesho saa tatu asubuhi, ili kutoa nafasi kwa kamati ya Bunge kukaa na kujadili suala hilo na kutafuta njia za haraka za  kuishauri serikali, badala ya kuruhusu wabunge waanze kuchangia hoja za serikali na tayari nina wachangiaji wengi hapa", alisema.

Akihutubia Bunge hilo kabla ya kuahirishwa Dkt. Nchimbi alisema  "Kamwe serikali haiwezi kuwafumbia macho wanasiasa wanaochochea vurugu hizi, watu wenye nia ya kuivuruga Tanzania, serikali imeshajipanga namna ya kudhibiti hali hiyo na kuleta utulivu kwa wakazi wa Mtwara", alisema Nchimbi.

Aliongeza kuwa "Katika kuhakikisha kwamba hali hiyo inathibitiwa ipasavyo tayari askari 32 wa Jeshi la Wananchi Tanzania(JWTZ) wamekwisha wasili mkoani Mtwara kutoka Nachingwea, kwa ajili ya kusaidia Jeshi la Polisi, kuna askari wetu wanne waliokufa katika ajali wakielekea Mtwara, hatuwezi kuacha damu zao zimwagike bure, kuna uharibifu mkubwa wa mali ikiwemo nyumba ya Mwandishi wa habari wa shirika la utangazaji Tanzania(TBC) pia imechomwa moto na kuteketea kabisa, haya yote hatuwezi kuyavumilia", alisisitiza Nchimbi.

No comments: