Wednesday, April 13, 2016

AHUKUMIWA MIAKA 30 JELA KWA KOSA LA UNYANG'ANYI WA KUTUMIA SILAHA




Na Steven Augustino,
Tunduru.

Yassin Raibu (31) ambaye ni mkazi wa kijiji cha Kazamoyo wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, amehukumiwa kutumikia kifungo cha miaka 30 jela baada ya kupatikana na kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha.

Adhabu hiyo ilitolewa na Hakimu mfawidhi wa Mahakama ya wilaya hiyo, Gladys Barthy baada ya Mahakama kujiridhisha na kutokuwa na mashaka dhidi ya ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri, ambao ulipeleka mashahidi saba kwa ajili ya kuthibitisha kosa hilo lililokuwa likimkabili.

Wakati huo Mahakama hiyo iliwaachilia huru watuhumiwa wengine wawili waliokuwa wanadaiwa kushirikiana na Raibu katika tukio hilo na kupora vitu mbalimbali vyenye thamani ya shilingi milioni 7,175,000 mali ya Said Khatib Yunusi, mkazi wa kijiji cha Lukumbule wilayani humo.


Walioachiliwa katika shauri hilo la jinai namba 44/2015 baada ya kufanyiwa upembuzi yakinifu na Mahakama hiyo na kuwaona kwamba hawana hatia ni Barali Shamte (41) mkazi wa kijiji cha Mavuji wilayani Rufiji na Fadhili Mangambila (43) mkazi wa kijiji cha Wenje wilayani Tunduru.

Awali akiwasomea shitaka hilo mwendesha mashtaka mkaguzi msaidizi wa Polisi Inspekta Songelael Jwagu aliiambia Mahakama kuwa katika tukio hilo, watuhumiwa hao wakiwa wanatumia bunduki aina ya SMG walimvamia Said Yunus na kumpora vitu mbalimbali vyenye thamani ya shilingi milioni 1.7.

Katika shkata hilo Inspekta Jwagu, alisema kuwa katika tukio hilo watuhumiwa hao waliiba fedha taslimu shilingi milioni 6,200,000, kamera aina ya Sony yenye thamani ya shilingi 300,000, walichukua simu sita za mkononi zenye thamani ya shilingi 425,000 pamoja na vocha za simu 2,500 za shilingi 1,250,000 majira ya saa 4.15 usiku Agosti 22 mwaka jana.

Akifafanua maelezo ya kosa hilo Inspekta  Jwagu alisema kuwa kwa kufanya tukio hilo watuhumiwa hao, walikiuka sheria namba 287 (a) ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Baada ya Mahakama hiyo kumtia hatiani, Inspekta Jwagu aliiomba Mahakama kuwapatia adhabu kali ili iwe fundisho kwa wengine ambao wamekuwa na tabia kama hiyo.

Alisema taarifa zinaonesha kuwa mtuhumiwa huyo ni miongoni mwa wahalifu sugu, ambaye alikwisha wahi kuhukumiwa na kupewa adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja jela baada ya kupatikana na hatia katika shauri la jinai namba 43/2015 baada ya kupatikana na kosa la kukutwa akiwa na bunduki aina ya SMG.

Raibu alipelekwa katika gereza la wilaya ya Tunduru na kuanza kutumikia adhabu ya kifungo  hicho kulingana na maelekezo yaliyotolewa na Mahakama hiyo.

No comments: