Saturday, April 9, 2016

WATOA DAWA MAGONJWA YALIYOSAHAULIKA TUNDURU WAPEWA ONYO



Na Steven Augustino, 
Tunduru.

WATOA dawa kwa ajili ya kinga na tiba ya magonjwa yaliyosahaulika, wilayani Tunduru mkoa wa Ruvuma, ambao wanajiona kwamba hawaendani na kasi ya utendaji kazi juu ya ugawaji wa dawa hizo, wametakiwa kujitoa mapema kabla hawajachukuliwa hatua za kisheria.

Hayo yamejitokeza kufuatia uwepo wa taarifa kwa baadhi ya wagawa dawa katika vijiji vya Nakapanya, Nalasi na vitongoji vyake wilayani humo ambapo kati yao wametishia kutaka kugomea zoezi hilo wakishinikiza waongezewe malipo ya ujira wa kufanya kazi hiyo.

Kaimu Katibu tawala wa wilaya ya Tunduru, Augustino Maneno alisema hayo wakati alipokuwa akimwakilisha Mkuu wa wilaya hiyo Chande Nalicho, kwenye zoezi la kuwaongoza baadhi ya wananchi ambao walijitokeza katika uzinduzi wa umezaji dawa hizo, uliofanyika hospitali ya wilaya iliyopo mjini hapa.

Magonjwa yaliyosahaulika na yale ambayo hayapewi kipaumbele (NTD) ni pamoja na magonjwa ya matende, mabusha, ngiri maji na ndiyo ambayo watu hupewa dawa ili yasiweze kuathiri afya zao.


Aidha katika uzinduzi huo Nalicho aliwataka wananchi wa wilaya hiyo kujitokeza kwa wingi kumeza dawa hizo zitakazowasaidia pia kwa ajili ya kinga na tiba ya magonjwa ya usubi, trakoma, kichocho na minyoo ya tumbo.

Mkuu huyo wa wilaya aliwataka wananchi kuondoa hofu na dhana potofu kwamba, dawa hizo zinapunguza nguvu za kiume na kuleta madhara ya aina mbalimbali.

Awali akisoma risala katika uzinduzi huo, Mratibu wa zoezi hilo ambaye ni mtaalamu wa magonjwa ya macho hospitali ya wilaya ya Tunduru, Zuhura Mshamu alisema tatizo linalochangia kuenea kwa magonjwa hayo linatokana na uchafu wa mazingira, ikiwemo uwepo wa mito mingi yenye maji yaendayo kasi hivyo kupelekea uwepo wa  mbu aina ya Qullex ambaye husababisha ugonjwa wa matende pamoja na inzi wadogo wanaoambukiza ugonjwa wa macho (Trakoma).

Zuhura alifafanua kuwa watu bilioni moja duniani, wameathirika na magonjwa hayo na watu bilioni mbili wapo hatarini kupata maambukizi ambapo kwa upande wa Tanzania, inakadiriwa kuwa zaidi ya watu milioni 43 wapo mbioni kuambukizwa  na watu milioni tano, wamekwisha athiriwa na mojawapo ya magonjwa hayo.

Akizungumza katika uzinduzi huo, naye Kaimu Mganga mkuu wa wilaya hiyo, Dkt. Vitalis Lusasi alisema zoezi hilo wilayani humo litaendeshwa katika zahanati na vituo vyote vya afya kwa kutoa dawa za kinga na tiba kwa magonjwa hayo ili yasiweze kuleta madhara katika jamii hapo baadaye.

No comments: