Wednesday, April 6, 2016

MHANDISI ASHINDWA KUTOLEA MAELEZO JUU YA UJENZI WA MADARAJA



Na Kassian Nyandindi,
Mbinga.

MHANDISI mkaguzi wa barabara na majengo Halmashauri ya mji wa Mbinga mkoani Ruvuma, Jordan Kapinga amejikuta akiwa katika wakati mgumu kufuatia Diwani wa kata ya Kitanda katika halmashauri hiyo, Zeno Mbunda kumtaka atolee maelezo juu ya kwa nini ujenzi wa madaraja na barabara umejengwa kwa kiwango cha chini ndani ya kata hiyo.

Hali hiyo ilifuatia baada ya Diwani huyo kuibua hoja hiyo, katika kikao maalum cha Wenyeviti na wazee wa vijiji vya kata hiyo kilichoketi kwenye ofisi za makao makuu ya kata ya Kitanda Aprili 2 mwaka huu, kwa lengo la kujadili maendeleo ya kata hiyo na kero mbalimbali zinazowakabili wananchi wake.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Akizungumza katika kikao hicho, Mbunda alisema kuwa ujenzi wa barabara na madaraja matatu ambao umefanywa katika kata hiyo haujashirikisha wananchi na mkandarasi husika aliyepewa kazi hiyo hakuripoti kwa uongozi wa kata hiyo jambo ambalo linawafanya wajenge shaka.

Kampuni ya Ndapa Interprises Corporation Company Limited kutoka Dar es Salaam, alisema kuwa ndiyo iliyopewa kazi hiyo ambapo ujenzi wa barabara na madaraja hayo umefanyika kwa kiwango cha chini.


Alifafanua kuwa daraja la mto Ruvuma, ambalo lilitengewa fedha shilingi milioni 43,970,000 na ujenzi wake ulikuwa ni wa kuanzia mwezi wa 6 hadi wa 12 mwaka 2015 Kandarasi huyo cha kushangaza, ameanza kwa kujenga nguzo tu na kutelekeza kazi hiyo.

Mbunda alibainisha kuwa alipofanya ufuatiliaji katika ofisi za ujenzi halmashauri ya mji wa Mbinga, taarifa zinaonesha kuwa mkandarasi huyo tayari alikwisha lipwa malipo ya awali shilingi milioni 13,194,000.

“Mnamo tarehe 11 mwezi Machi mwaka huu, nilikwenda kuwaona wataalamu wa ujenzi walinihakikishia ujenzi wa daraja hili utafanyika lakini mpaka sasa hakuna kazi iliyofanyika, na mhusika aliyepewa kazi ya ujenzi wa miundombinu hii hajaripoti katika ofisi ya kata yangu tokea apewe kazi hizi ”, alisema Kapinga.

Akizungumzia kwa upande wa ujenzi wa barabara katika kata hiyo, alisema kuwa makalvati yaliyojengwa na kufukiwa barabarani yamebomoka huku maeneo yaliyokuwa korofi ambayo yalikwanguliwa na greda, alililopitisha wakati wa ujenzi huo yamebomoka hali ambayo inaonesha kwamba ujenzi wake ulikuwa ni wa kiwango cha chini.

Kwa upande wao Wenyeviti na wazee hao kwa nyakati tofauti nao waliibua hasira zao, wakiiomba serikali ichukue hatua ya kumkamata na kumshtaki Mahakamani mkandarasi huyo ambaye ameshindwa kufanya kazi aliyopewa na kusababisha kero kwa wananchi.

“Sisi tunataka tupate majibu ni lini huyu mtu amechukuliwa hatua na Rais wetu John Magufuli apokee kilio chetu juu ya matatizo haya, tunasema mkandarasi huyu ni mwizi tena ameingia katika kata yetu bila kutoa taarifa mradi ameujenga chini ya kiwango”, alisema Castory Ndunguru Mwenyekiti wa baraza la wazee kata ya Kitanda.

Vilevile Amon Ndunguru ambaye ni Mwenyekiti wa kijiji cha Masimeli katika kata hiyo, aliongeza kuwa dalili hizi zinadhihirisha wazi kuwa mchakato wa tenda juu ya upatikanaji wa kazi hizo alizopewa mkandarasi hazikufuatwa, ikiwemo wananchi waliopo katika eneo husika ambako mradi unatekelezwa kwanza ilibidi washirikishwe ili kuondoa malalamiko yasiyokuwa ya lazima.

Mhandisi mkaguzi wa barabara na majengo Halmashauri ya mji wa Mbinga, Jordan Kapinga aliposimama katika kikao hicho ili aweze kutolea ufafanuzi juu ya malalamiko hayo kwanza alikiri juu ya diwani wa kata ya Kitanda Zeno Mbunda kwenda kwenye ofisi za ujenzi za halmashauri hiyo, kufuatilia kero hizo huku akiongeza kuwa yeye wakati miradi hiyo inajengwa hakushirikishwa mchakato wake hivyo hawezi kutolea majibu sahihi, kwa sababu jambo hilo lipo nje ya uwezo wake.

No comments: