Tuesday, April 26, 2016

DED LUSEWA APIGA MARUFUKU VIJANA KUFANYA MAANDAMANO YASIYOKUWA YA LAZIMA



Na Muhidin Amri,
Namtumbo.

MKURUGENZI mtendaji wa Mamlaka ya mji wa Lusewa, wilayani Namtumbo mkoa wa Ruvuma Astery Mwinuka, amepiga marufuku tabia ya vijana kufanya maandamano yasiyokuwa ya lazima pindi wanapodai haki zao, badala yake wafuate sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa ikiwemo kutumia Ofisi ya Mamlaka hiyo katika kutafuta majawabu ya kero zao mbalimbali zinazowakabili.

Mwinuka alitoa onyo hilo, mara baada ya kukabidhiwa rasmi  majengo  yatakayotumika kama Ofisi za Mamlaka ya mji wa Lusewa katika sherehe fupi iliyofanyika hivi karibuni na kuhudhuriwa na wananchi wa kata tatu za Lusewa, Msisima na Magazini ambazo kwa pamoja zimeunda mamlaka hiyo.

Alisema kuwa tayari serikali imesikiliza kilio chao  kwa kuanzisha mamlaka ya mji huo ambayo itakuwa na dhamana ya kusimamia shughuli zote za maendeleo, kutatua kero na kukabiliana na changamoto mbalimbali, hivyo ni vyema wananchi wakawa na utaratibu wa kupeleka kero zao katika ofisi hizo badala ya kuanzisha migogoro isiyokuwa na tija kwao.

“Tumepata mamlaka ya mji kamili hapa Lusewa, natoa onyo kali kuanzia sasa hakuna tena maandamano ambayo yatawapotezea muda wenu wa kufanya kazi kama kuna tatizo  tumieni ofisi za mamlaka na sio kukimbilia kwa mkuu wa wilaya, mtapoteza muda wenu wa kufanya kazi na wengine mtajikuta mkiishia mikononi mwa vyombo vya dola”, alisema Mwinuka.


Aidha amepiga marufuku, vijana kutumia saa za kazi kucheza mchezo wa Pool au kuzungumzia mambo ya siasa, badala yake amewataka watumie muda wao katika kufanya kazi za uzalishaji mali hususani kilimo ambacho kina nafasi kubwa ya kumaliza tatizo la umaskini  katika familia zao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Namtumbo, Danny Nyambo amewataka wakazi wa kata ya Lusewa na maeneo jirani kuhakikisha kwamba wanatoa  ushirikiano wa kutosha kwa watumishi hao, ili mamlaka hiyo iweze kutekeleza na kufanya kazi zake kwa ufanisi mkubwa.

Nyambo alibainisha kuwa kuanzishwa kwa mamlaka hiyo ni jambo la faraja kwa wananchi wote wa wilaya ya Namtumbo, kwa kuwa itasaidia kuharakisha upatikanaji wa maendeleo ya mtu mmoja mmoja, halmashauri na mkoa wa Ruvuma kwa ujumla.

No comments: